Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetumia muda wa saa moja kukusanya zaidi ya Sh9 milioni.
Chama hicho kilikusanya kiasi hicho cha fedha
katika saa moja tangu kuzindua Programu ya Siasa Mtandaoni, iliyofanyika
jana jijini humo na kilizindua vipengele vitatu, kikiwamo cha
uchangishaji fedha kutoka kwa wananchi ili kukisaidia katika harakati za
kuikomboa Tanzania huru.
“Zaidi ya Watanzania milioni 20 wanatumia simu za
mkononi hapa nchini. Tunaomba watumie simu hizohizo kuichangia Chadema
kutekeleza majukumu yake. Vodacom wako tayari na tutaanza nao leo wakati
tukiwasubiri Airtel na Tigo, ambao wataanza Jumatano ijayo.
Mfumo huu wa kuchangia utakuwa na uwezo wa kutunza
kumbukumbu za wote waliochangia na kama watapenda kuonekana au la
wataweza kufanya hivyo,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe.
Mifumo mitatu iliyozinduliwa jana ni malipo kwa
njia ya mtandao (e-payment), kujisajili uanachama kwa njia ya mtandao
(e-membership) na upataji wa taarifa za chama kupitia simu ya mkononi
(Chadema media) ambayo inahitaji mhusika kujiandikisha.
Hatua hiyo inaifanya Chadema kuwa chama cha kwanza nchini kuleta mapinduzi ya teknolojia kwenye siasa.
Uzinduzi huo ulifanyika saa 5 usiku, huku
uchangiaji ukipewa kipaumbele, ambapo Mbowe alitoa maelekezo kwa
Watanzania wote waliokuwa wakilifuatilia tukio hilo kupitia runinga zao.
Mara baada ya maelekezo kutolewa, wachangiaji
walikuwa wengi hata kusababisha mfumo kuelemewa kutokana na idadi hiyo
kuzidi uwezo wake.
Uchangiaji ulikuwa mkubwa ndani ya dakika kumi za mwanzo, huku ukipungua kadri muda ulivyozidi kwenda.
Katika dakika nne za mwanzo zaidi ya Sh4.7 milioni
zilichangwa, kiwango ambacho kiliongezeka kufikia zaidi ya Sh6.798
milioni katika dakika ya 8 na dakika moja baadaye tayari kulikuwa na
zaidi ya Sh7.6 milioni.
Hadi sherehe hizo zilipohitimishwa na viongozi wa
kitaifa wa chama hicho kuondoka ukumbini saa 6:00 usiku, michango hiyo
kupitia Mpesa ilikuwa imefikia Sh9,262,041.
Baada ya uzinduzi huo, chama hicho kilianza
kupokea michango kutoka kwa marafiki na wanachama wa mikoani pamoja na
vyama rafiki vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi na jumla ya Sh56.42
milioni pamoja na Dola700 za Marekani zilikusanywa.
Wachangiaji hao walipata nafasi ya kushikana mikono na
mwenyekiti wa chama pamoja na viongozi wengine ambao ni Katibu Mkuu, Dk
Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika pamoja na Makamu
Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed.
“Hatuupendi umaskini, lakini tunawapenda maskini
wote wa nchi hii. Waliopo madarakani wameupaka rangi umaskini na kila
asemaye kuwa ni mtoto wa mkulima anaonekana anafaa. Haya ni matusi kwa
wakulima wa nchi hii kwa kuwa kinachowakwamisha ni sera mbovu
zilizowekwa na watungaji hao ambao hawana uchungu na maisha ya watu wa
chini,” alisema Mbowe.
No comments:
Post a Comment