SOUTHAMPTON inatingisha kwenye Ligi Kuu England kwa kushika
nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 22,
pointi nne nyuma ya vinara Chelsea.
Kabla ya mechi za juzi, Jumapili kwenye tano bora
kulikuwa na kikosi cha West Ham United pia na kushangaza wengi kutokana
na mwenendo wa ligi hiyo ulivyo baada ya kuchezwa kwa mechi takribani
10.
Hata hivyo, makocha wa timu hizo zinazoshangaza
kwa kushika nafasi za juu hawapo kwenye orodha ya mameneja watano
wanaolipwa mishahara mizuri zaidi kwenye ligi hiyo.
Makala haya yanazungumzia makocha watano wanaolipwa vizuri zaidi kwenye Ligi Kuu England.
Brendan Rodgers (Liverpool, Pauni 3.25 milioni)
Kikosi chake cha Liverpool kwa sasa kinayumba, mambo hayaendi vizuri kutokana na kucheza chini ya kiwango.
Kufanya vizuri kwa klabu hiyo kwa msimu uliopita
na kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kulimfanya Brendan
Rodgers kupata dili la maana Anfield baada ya kusaini mkataba
unaomshuhudia akilipwa Pauni 3.25 milioni kwa mwaka na kuwa kocha
anayelipwa vizuri kwenye ligi hiyo.
Manuel Pellegrini (Man City, Pauni 3.47 milioni)
Ni kitu kinachoweza kukushangaza kidogo hasa kwa hadhi iliyonayo katika Klabu ya Manchester City.
Man city wakiwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu
England, kocha wake halipwi pesa nyingi sana kwa kulinganisha na makocha
wengine wa klabu kubwa.
Bosi huyo raia wa Chile, kwa mwaka amekuwa alipokea Pauni 3.47 milioni kutokana na huduma yake anayoitoa klabuni Etihad.
Arsene Wenger (Arsenal, Pauni 6.89 milioni)
Mfaransa huyo wa Arsenal anashika nafasi ya tatu kwenye orodha ya makocha wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye Ligi Kuu England.
Wenger, ambaye Mei mwaka huu alisaini mkataba wa
miaka mitatu wa kuendelea kuinoa klabu hiyo ya Emirates kwa huduma yake
anayotoa kwenye kikosi hicho kwa mwaka analipwa Pauni 6.89 milioni.
Louis van Gaal (Man United, Pauni 7 milioni)
Kazi yake kubwa ya kwanza klabuni Manchester United ni kuirudisha timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Mdachi huyo amechukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo
ya Old Trafford msimu huu baada ya kufukuzwa kwa David Moyes, ambaye
aliisababisha timu kuboronga kwenye msimu uliopita na kukosa nafasi ya
kucheza soka la Ulaya.
Kwenye ajira yake mpya Old Trafford baada ya
kutoka kuinoa timu ya taifa ya Uholanzi, Van Gaal amekuwa akilipwa
mshahara wa Pauni 7 milioni kwa mwaka.
Jose Mourinho (Chelsea, Pauni 8.37 milioni)
Anatajwa kuwa mmoja wa makocha wenye mafanikio
katika kizazi cha kisasa akiwa kwenye daraja moja sambamba na Pep
Guardiola wa Bayern Munich.
Kocha huyo wa Chelsea, amekuwa akifanya vizuri
katika kila klabu anazopita kuzifundisha na mwaka jana aliporejea kuinoa
timu hiyo ya Stamford Bridge akitokea Real Madrid.
Mourinho alisaini mkataba unaomfanya apokee kiasi
cha Pauni 8.37 milioni kwa mwaka na kuwa kocha anayelipwa pesa nyingi
zaidi kwenye Ligi Kuu England.
No comments:
Post a Comment