Serikali za China na Tanzania, zimetoa matamshi
makali dhidi ya kile zilichokiita “taarifa za uongozi na uzushi” ambazo
zinahusisha ndege ya Rais wa China, Xi Jinping na usafirishaji wa
vipande vya meno ya tembo kutoka Tanzania.
Jana kwa nyakati tofauti, Balozi wa China hapa
nchini, Lu Youqing, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu walitoa
taarifa wakituhumu taasisi iliyotoa ripoti hiyo kwamba malengo yake ni
kuharibu uhusiano mwema baina ya nchi hizo.
Ripoti ya taasisi ya Uingereza iitwayo
Environmental Investigation Agency – EIA (Wakala wa Uchunguzi wa
Mazingira) iliyotolewa juzi, inawatuhumu maofisa na wanausalama
waliokuwa katika msafara wa Rais Jinping wakati wa ziara yake nchini
Tanzania Machi 2013, kwamba walitumia fursa ya kidiplomasia kusafirisha
vipande vya meno ya tembo katika ndege ya rais.
Hata hivyo, Balozi Youqing aliliambia waandishi wa habari
mjini Arusha kuwa taarifa hizo zimetolewa na watu wasiopenda maendeleo
ya nchi maskini na kuongeza: “Ni uongo, uongo mkubwa, kama angejitokeza
hadharani mtu kama huyo anastahili kuadhibiwa vikali na mwongo ni lazima
aadhibiwe.”
“Taarifa hizi za uongo na zisizo na chembe ya
ushahidi zimetolewa na watu wasiopenda maendeleo ya nchi maskini kama
Tanzania,” alisema Balozi Youqing baada ya ufunguzi wa Mkutano wa
Kimataifa wa Kuzuia Ujangili unaoendelea jijini Arusha.
Alisema tuhuma hizo zimetolewa na watu wasio na
ushahidi na kwamba lengo lake ni kuharibu jina na sifa ya taifa lake
mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Kauli bungeni
Mjini Dodoma Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe alitoa kauli ya Serikali bungeni akisema
tuhuma dhidi ya msafara wa Rais Jinping hazina ukweli wowote na kwamba
hata madai kuwa serikali haijali wala haichukui hatua dhidi ya
wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo siyo za kweli.
“Taarifa za taasisi ya EIA ni za kupikwa na
kuungwaungwa ili kuchafua heshima ya nchi yetu, pamoja na kuchafua
heshima ya rafiki zetu wa China,” alisema Membe na kuongeza: “Ni taarifa
iliyoandaliwa na kutolewa wakati huu kukidhi ajenda mahususi ambayo
tunaifahamu fika.”
Membe alisema mtoa taarifa ambaye ametajwa kuwa
chanzo cha habari ni mtu mmoja ambaye walimkuta barabarani na kuanza
kumuuliza maswali wakati mtu huyo siyo mtumishi wa bandari wala uwanja
wa ndege.
“Ni mpitanjia tu wa mitaani. Hata video ya mahojiano inaonyesha hivyo,”alisema Membe.
Kwa upande wake, Waziri Nyalandu alisema uhusiano
wa Tanzania na China ni wa muda mrefu na kuheshimika kiasi kwamba
taarifa hizo zimeisononesha serikali. “Tunakamata Wachina wengi sana kwa
tuhuma za kukutwa na meno ya tembo, lakini hii ya ndege ya Rais ni
matusi,”alisema
Ukaguzi wa ndege
Nyalandu alisema ni kweli kwamba Wachina wamekuwa
wakihusishwa na biashara ya meno ya tembo na wamekamatwa wengi, lakini
kuhusisha ndege ya Rais wa China ni uongo kwani ndege hizo hukaguliwa na
maofisa usalama wa pande zote.
Balozi Youqing akizungumzia suala hilo alisema
Tanzania imefanya kazi nzuri katika kupambana na ujangili na kwamba
inasikitisha kusikia inahusishwa na masuala ambayo si ya ukweli, kwani
hata msafara wa viongozi wa nchi hizo hukaguliwa kabla ya safari.
“Mimi ndiye niliyeratibu safari nzima wakati wa
ziara ya Rais, hivyo ningejua kinachotokea, kwani hata mimi mwenyewe
nilikuwa nakaguliwa na maofisa wa usalama wa China na wa Tanzania,
isingewezekana,” alisema Balozi Youqing.
Ziara ya Jinping
Akizungumzia zaidi ziara ya Rais Jinping, Membe
alisema ilikuwa ya saa 24 na programu yake ilianza mara tu alipowasili
nchini na kutokana na ratiba ilivyokuwa kwa rais na wajumbe wake
isingewezekana ununuzi wa aina yoyote kufanywa na ujumbe huo.
“Alianza na dhifa ya kitaifa, akaenda kuzindua
ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, akawa na mkutano na
Rais wa Zanzibar pia na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa baada ya hapo
walikwenda kwenye makaburi ya Wachina kule Majohe na kisha kuondoka
kwenda uwanja wa ndege. Sasa hizo ‘shopping’ zilifanyika saa ngapi?”
alihoji Membe.
Alisema ni muhimu kujiuliza kwa nini taarifa hizo
zitoke leo hasa baada ya ziara ya Rais Jakaya Kikwete nchini China na
kwa nini ije baada ya Rais kuhutubia mafanikio ya ziara hiyo.
“Jibu kila mmoja anaweza kujua. Wasambazaji wa
taarifa hizi hawaitakii mema nchi yetu. Hawawatakii mema marafiki zetu
wa China. Wamejawa na wivu na husuda kwa mafanikio ya China na
inashangaza kuona wanawachukia huku wanawategemea,” alisema Membe.
Kauli yake inaungwa mkono na ile ya Nyalandu ambaye alisema:
“Rais wa China alikuwa katika ziara ya pili tangu
aingie madarakani baada ya kwenda Urusi na akaja Tanzania ambako alitoa
mwelekeo wa serikali yake katika uhusiano wa nchi yake na Afrika”.
Alisema hii ni mara ya pili kwa vyombo vya habari
vya nje kutoa taarifa mbaya kuhusu Tanzania kabla ya kuanza kwa mikutano
mikubwa kimataifa kuhusiana na majangili, akirejea habari zilizoandikwa
na Daily Mail la Uingereza siku moja kabla ya Rais Kikwete kuhudhuria
mkutano nchini Uingereza.
“Leo wamejua kutakuwa na mkutano mkubwa kama huu na masikio ya watu yakielekezwa Arusha ndiyo habari hii inatoka.”
Mkutano wa Arusha
Awali akizungumza katika mkutano wa kutokomeza
ujangili, Balozi Youqing aliitaka serikali ya Tanzania kuanza kutoa
adhabu kali kwa watu wanaojihusisha na ujangili.
Alisema nchini China wanaokutwa na hatia ya makosa kama hayo adhabu yao huwa ni kunyongwa hadi kufa.
Balozi huyo alisema Serikali yake imekuwa ikitoa
misaada ya fedha na utaalamu katika kukabiliana na ujangili nchini
Tanzania na kuwa mafanikio yameanza kuonekana.
Naye Nyalandu alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kimataifa imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokomeza ujangili.
“Matokeo makubwa yamepatikana na katika kipindi
kifupi, kwani kwa miezi minne sasa Tanzania inaweza kujivuna, kwani
hakuna tembo hata mmoja aliyeripotiwa kuuawa katika pori la akiba la
Selous,” alisema Waziri Nyalandu.
Mkutano huo wa kikanda unajadili mbinu za
kupambana na ujangili na utoroshwaji wanyama katika nchi za ukanda wa
Bahari ya Hindi, Afrika Mashariki na Sudan Kusini.
No comments:
Post a Comment