Friday 21 November 2014

Mwanafunzi abakwa darasani

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mwanafunzi anayesoma kidato cha kwanza katika Sekondari ya Ntunduru, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza (jina linahifadhiwa), mwenye umri wa miaka 14, ameumizwa vibaya sehemu za siri na shingoni baada ya kubakwa akiwa shuleni.
Tukio hilo limetokea Novemba 15, mwaka huu, saa nane mchana ambapo mwanafunzi huyo alibakwa katika moja ya vyumba vya madarasa shuleni hapo na kabla ya kufanyiwa kitendo hicho, wabakaji walimziba mdomo kwa kumkaba shingoni.
Habari zilizotufikia  zinasema kuwa, baada ya mwanafunzi huyo kuingia katika chumba cha darasa hilo ambacho kilikuwa na wanafunzi wawili wa kidato cha nne, ambapo mmoja wao alimkaba shingo, kumziba mdomo na mwenzake alimvua nguo na kuanza kumfanyia kitendo hicho cha kikatili.
Baada ya wabakaji hao kufanya tukio hilo, walikimbia na kumuacha mwanafunzi huyo akipiga kelele ili kuomba msaada wa wenzake bila mafanikio.
Akizungumzia tukio hilo huku akitokwa machozi, Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Bi.Careen Yunus, alisema atahakikisha wahusika wa ukatili huo wanakamatwa kwani kitendo hicho hakikubaliki wala kuvumilika.
“Ni muhimu kujua wanafunzi wa kike katika shule hii ambayo ni ya bweni inayomilikiwa na mtu binafsi wapo salama kiasi gani kutokana na mazingira ya tukio lenyewe tena limetokea mchana baadhi ya walimu wakidaiwa kuwepo shuleni,” alisema.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo (jina tunalihifadhi), alisema msukumo wa Bi. Yunus ndiyo uliomsaidia kufanikisha utekelezwaji wa hatua za kisheria ukiwemo uchunguzi kwani awali alikumbana na vikwazo vya kukosa ushirikiano kwa baadhi ya walimu.
“Inauma na inasikitisha sana, huu ni ukatili wa aina yake na kinachonishangaza, mwanangu amefanyiwa ukatili huu ndani ya mazingira ya shule tena mchana,” alisema mama huyo.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Bahati Charles, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini aliomba kutoingia kwa kina akidai tayari lilikuwa linafanyiwa uchunguzi na vyombo vya dola.
“Ni kweli tukio hilo limetokea kama inavyodaiwa lakini halikuchangiwa na menejimenti ya shule bali ni tabia ya vijana wa leo kukosa maadili,” alisema Bw. Charles.
Polisi wilayani Sengerema wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kufunguliwa jalada SENG/RB/2949/2014 ambapo watuhumiwa ni Sayila Kitayata anayedaiwa kumsaidia mtuhumiwa aliyebaka kwa kumkaba shingo mwanafunzi huyo na kumziba mdomo wakati Christian Mwita akifanya ukatili huo na wote kukimbia.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Valentino Mlolowa, naye amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akidai jeshi hilo linaendelea kuwasaka watuhumiwa kwani vitendo vya aina hiyo havivumiliki.

No comments: