Tuesday, 18 November 2014

Emeh Izuchukwu akaribia kutua Simba

Straika namba moja wa Elverum FC ya Norway, Minigeria
Simba inaweza kumalizana na straika namba moja wa Elverum FC ya Norway, Minigeria Emeh Izuchukwu. Mchezaji huyo akiwa na mwenzake, Orji Obinna, waliwahi kutamba na Simba mwaka 2008 wakitokea Enyimba ya kwao Nigeria.
Wachezaji hao waliondoka nchini kwenda kusaka noti Ulaya, lakini sasa Emeh amefanya mazungumzo ya kina na Simba na wakati wowote wiki hii anaweza kumalizana nao na kutua nchini,
Mbali ya hao, pia Simba imewapandisha ndege wachezaji watatu kutoka jijini Mbeya kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na kuwasainisha mikataba. Wachezaji hao ni beki wa kati Nurdin Chona na beki wa kulia Salum Kimenya wote kutoka Prisons ambao walitua jijini Dar es Salaam Jumamosi wakati mshambuliaji wa Mbeya City, Deus Kaseke, aliingia jana Jumatatu.
Taarifa za kuaminika ambazo tumezipata jana Jumatatu ni kwamba vigogo wa Simba walikutana na mchezaji mmoja mmoja kwa nyakati tofauti ambapo ilielezwa kwamba Chona ametaka dau la Sh 30 milioni, Kimenya ameanzia Sh25 milioni huku Kaseke akitaka kupewa Sh40 milioni, hata hivyo vigogo hao wamesema kwamba kwao fedha sio tatizo.
Wachezaji hao ni mapendekezo ya viongozi baada ya kocha wao Patrick Phiri kutoa baraka kwa viongozi kumsaidia kusaka wachezaji wazuri kwa maelezo kwamba bado hawajui vizuri wachezaji wote wenye viwango vya juu vya kuichezea Simba huku wakipendekeza pia jina la Said Morad wa Azam FC.
Phiri yeye katika ripoti yake aliyoikabidhi alipendekeza majina ya wachezaji wa Mtibwa Sugar mshambuliaji Ame Ally na beki Hassan Kessy, Danny Mrwanda (Polisi Moro) na Dan Sserunkuma wa Gor Mahia ya Kenya ambaye tayari wameshaanza mazungumzo. Hata hivyo uwezekano wa kumpata Mrwanda ni mdogo kwani anarudi Vietnam alikokuwa akicheza soka la kulipwa.
Phiri alitaka pia atafutiwe wachezaji wa nafasi mbalimbali ikiwemo beki ya kulia na kushoto, beki ya kati, kiungo, straika na kipa ambapo imedaiwa kuwa Juma Kaseja atarejea Simba wakati wowote kwani tayari amevunja mkataba wake na Yanga.
Kwa upande wa viongozi wa Simba walisema wamezungumza na wachezaji wengi hasa nafasi ya straika na beki na wanaamini watafanikiwa kwa asilimia kubwa.
Simba ndiyo timu pekee inayoonekana kuhaha kwenye usajili wa dirisha dogo kuhakikisha inapata wachezaji wazuri kutokana na matokeo yao waliyoyapata katika mechi saba za kwanza za Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo ilitoka sare mechi sita na kushinda mechi moja tu. Ipo katika mpango wa kuwatema wachezaji wake kadhaa akiwemo Uhuru Seleman, Ivo Mapunda, Amri Kiemba ambaye Azam wanamhitaji.
Wengine ni Mrundi Pierre Kwizera anayedaiwa kupelekwa kwa mkopo Afrika Kusini pamoja na Joram Mgeveke anayetafutiwa timu ya mkopo, Nassoro Masoud ‘Chollo’ na Haruna Chanongo ambao wanatajwa kuachwa kutokana na madai ya kushuka kwa viwango vyao.

No comments: