Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limemtia mbaroni mganga
mmoja wa jadi anayedaiwa kuteka watoto kwa njia za kishirikina kwa ajili
ya kutolewa kafara.
Mbali na mganga huyo, pia wamemtia mbaroni
mwanamke mmoja, anayedaiwa kusuka mipango ya kutekwa nyara kwa watoto na
kuwahifadhi kwa mganga huyo.
Mganga huyo ambaye anadaiwa ni mwenyeji wa mkoani
Mbeya, alikutwa na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13, akiwa tayari
amepumbazwa tayari kumpeleka Mbozi mkoani Mbeya. Mtoto huyo aliyemaliza
darasa la saba mapema mwaka huu Shule ya Msingi Majengo katika Manispaa
ya Moshi ni miongoni mwa waliofaulu katika mtihani wa Taifa.
Kwa mujibu wa habari hizo, mganga huyo (jina
tunalo), anadaiwa kushirikiana na mwanamke mmoja, mkazi wa TPC kula
njama za kumteka mtoto huyo. “Huyo mwanamke ndiye alishirikiana na huyo
mganga kumteka mtoto kwa lengo la kumpeleka Mbozi, mkoani Mbeya na ajabu
ni kwamba naye alikuwa akishiriki kumtafuta,” imedokezwa.
Kulingana na chanzo hicho, kiini cha kugundulika
kwa mpango huo ni baada ya mwanamke huyo kwenda na rafiki yake kwa
mganga, ikiwa ni maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kusafiri.
“Walipeleka chakula kwa huyo mganga na walipoingia
ndani ndipo rafiki yake akamuuliza mbona huyu mtoto, ndiye
anayetafutwa,” alidokeza mmoja wa ndugu wa mtoto na kuongeza:
“Huyo mwanamke ndiyo akamwambia naomba unyamaze
kwa sababu huyu mtoto anasafiri kwenda Mbozi na mganga na wazazi wake
hawatakaa wamwone tena na ndiyo maana nimeleta na hili begi.”
Hata hivyo, rafiki huyo aliamua kuvujisha siri
hiyo kwa ndugu wa mtoto huyo kuwa amefichwa nyumbani kwa mganga huyo na
ndipo ndugu walipomfuata kwa mganga.
Akizungumza na gazeti hili nje ya kituo cha kati
cha polisi mjini Moshi, Prosper Swai ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo,
alisema mwanaye alitoweka Novemba 2 na baada ya kutoonekana alitoa
taarifa kituo cha Polisi cha TPC na kwa uongozi wa kijiji na juhudi za
kumtafuta hazikuzaa matunda.
Swai alisema baada ya siku tano, alipata taarifa
kwa mtu mmoja kuwa mwanae amehifadhiwa nyumbani kwa mganga na alipelekwa
na mwanamke huyo.
Baada ya kupata taarifa hizo, akiwa na polisi na
uongozi wa kijiji, walivamia nyumba ya mganga huyo na kumkuta mtoto
akiwa amelala chini kwenye mfuko wa mbolea akiwa hajitambui.
Alifafanua kuwa baada ya kumpata mtoto huyo,
alimkagua na kumkuta na hirizi kubwa kiunoni hali iliyomfanya aogope
kuwa mwanae huyo aliibwa kwa lengo la kutolewa kafara.
Swai alisema matukio ya wizi wa watoto katika eneo la TPC na
maeneo ya jirani yamekithiri na katika kipindi cha mwezi mmoja, watoto
wanne wamepotea katika mazingira hayo.
Alisema wawili kati yao ni wakazi wa Kijiji cha
Langasani na walikutwa wamekatwa viungo na kutupwa msituni wakati mtoto
mwingine ni wa Kijiji cha Chekereni ambaye bado hajapatikana.
Mtoto mwingine ni wa Kijiji cha Mbugani alitoweka
juzi baada ya baba yake kumtuma kwenda kukagua tanuru la matofali na
hadi jana mchana alikuwa hajapatikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey
Kamwela alikiri kumshikilia mganga huyo na watu wengine wanaodaiwa
kuhusika kumpeleka mtoto huyo kwa mganga huyo na kuwa atatoa taarifa
baada ya kukusanya taarifa zaidi.
No comments:
Post a Comment