uongozi wa Azam umemfungulia milango kiungo mshambuliaji wa
Yanga, Haruna Niyonzima, huku ukipanga kumfukuza Mhaiti Leonel
Saint-Preux aliyeshindwa kuonyesha kiwango cha juu kama ilivyotegemewa.
Azam ilimsajili mshambuliaji huyo kabla ya
mzunguko wa kwanza wakiwa na matumaini kuwa angeshirikiana na John
Bocco, Kipre Tchetche, Didier Kavumbagu kutengeneza safu kali ya
ufungaji wa mabao msimu huu.
Mwenyekiti wa Azam, Said Mohamed ‘Mzee Said’
alisema jana kuwa kimsingi Niyonzima ni mchezaji wao, walishamsainisha
mkataba kabla hajatua Yanga, hivyo wanataka kumrudisha nyumbani.
Mohamed aliliambia gazeti hili jana kuwa wanajua
matatizo yote anayokumbana nayo raia huyo wa Rwanda ndani ya Yanga,
hivyo iwapo ni wakati mwafaka wa kumrejesha kundini.
“Mkataba wa mwanzo kabisa wa Niyonzima tunao, ila
tulimruhusu ajisajili Yanga kwa vile kocha Stewart Hall (wakati ule)
alimkataa akisema ni mfupi.
“Niyonzima ni mchezaji mstaarabu,hana tamaa, hata
mkataba wake wa mwanzo ulipoisha Yanga akatuambia arudi, yeye bado ana
mapenzi na Azam, ila sisi tulimwambia aendelee kubakia Yanga.
“Tumesikia kwa sasa ana matatizo na klabu yake, ni
wakati mwafaka wa kumrudisha nyumbani, milango yetu ipo wazi
tunachofanya kwa sasa ni kuzungumza na kocha (Joseph Omog) ili
tumsajili,”alisema
Alisema iwapo kocha wao ataridhia wamsajili Niyonzima , watamwondoa Leonel Saint-Preux.
Kauli hiyo ya Mohamed kuhusu kiungo huyo
Mnyarwanda imekuja huku mchezaji huyo akikaririwa katika siku za
karibuni akilalama kwamba amekuwa akiishi maisha magumu ndani ya Yanga
kwa kile anachodai kuchukiwa na kocha Marcio Maximo.
Amekuwa akidai kuwa Maximo amekuwa akimtoa katika
mechi za Ligi Kuu kabla ya dakika 90, kitu ambacho kimekuwa kikimuudhi
kiasi cha kumshushia lawama kocha wake kuwa hamthamini.
Wakati huohuo, Mohamed alisema mahitaji ya kocha wao Azam yapo wazi.
“Kocha anataka nafasi tatu, beki ya kati, kiungo
na mshambuliaji, awali tulimtaka Amri Kiemba tukawaomba Simba tumnunue
wakatukatalia, wakasema tuandike barua tumchukue kwa mkopo, tumeandika
barua kama walivyoagiza sasa hivi wamegeuka wanataka tumnunue moja kwa
moja.
“Tatizo viongozi wa Simba wanavurugana wenyewe, hawaelewani wapo
wanaotaka auzwe, wapo wanaotaka asiuzwe, tumeamua kuangalia sehemu
nyingine, iwe klabu za daraja la kwanza, au ligi kuu ilimradi awe ni
mchezaji mzuri tutamchukua kwa garama yoyote.
Tulimtolea macho Jonas Mkude, laiti Simba
ingezubaa kidogo, basi tungemchukua, sisi na Yanga nao walikuwaa
wanavizia mawindo,” alisema.
No comments:
Post a Comment