STRAIKA aliyechukua hatamu kwenye fowadi ya Simba, Mganda
Emmanuel Okwi, amesisitiza kwamba hana tofauti na mchezaji yeyote wa
Simba na anatamani kucheza pamoja na mshambuliaji anayeanzia benchi,
Mrundi Amissi Tambwe.
Thamani ya Tambwe ambaye alikuwa straika namba
moja wa Simba msimu uliopita, imeshuka kutokana na mfumo wa kocha
Mzambia Patrick Phiri ambao umemfanya aanzie benchi ingawa katika mchezo
wa Jumapili dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa ana nafasi
kubwa ya kuanza.
Tambwe ambaye alikuwa mfungaji bora msimu
uliopita, sasa anaanzia benchi na Phiri anapenda kumtumia zaidi Okwi kwa
maelezo kwamba ana kasi, nguvu na anajua kutumbukiza mipira nyavuni
tofauti na staili ya Tambwe ambaye ni mviziaji na akikutana na mabeki
wabishi timu hukwama.
Ingawa uongozi umekanusha kwa nguvu, lakini
kumekuwa na maneno kwamba thamani ya Tambwe ndani ya Simba imeshuka
baada ya Okwi kutua na kwamba mchezaji huyo anafikiria kuingia mitini
kwenye dirisha dogo la usajili litakaloanza Novemba 15 licha ya kwamba
uongozi unajitahidi kumuweka fiti kisaikolojia.
Okwi aliyetua Simba akitokea Yanga aliyositisha
nayo mkataba, alisema hana tatizo katika kucheza na Tambwe katika kikosi
cha kwanza na Phiri amekiri kwamba atawapanga.
Okwi alisema anapocheza na Tambwe katika kikosi
kimoja safu ya ushambuliaji yao inakuwa na makali zaidi. “Sina tatizo
katika kucheza na Tambwe pale mbele wala mchezaji mwingine yeyote,
nakumbuka kuna mechi tuliyocheza pamoja mimi na Tambwe tulielewana sana
nikajikuta nimebanwa na mabeki lakini Tambwe akawa sehemu safi nikampa
krosi akafunga kirahisi kabisa,”alisema Okwi ambaye amekuwa akijituma
sana katika mechi za hivikaribuni mpaka kufikia hatua ya kucheza na
majeraha.
Kwa upande wake Phiri alisema: “Kuna mechi
nakumbuka walicheza pamoja Tambwe akafunga, lakini hapa kati sikuwa
nawapanga pamoja kuna mambo nilikwa najaribu kuyapanga sasa Okwi anaumwa
lakini akipona tutaangalia uwezekano wa kuweza kuwatumia tena kucheza
pamoja katika mechi ijayo.”
Katika mazoezi ya juzi Jumatano ya kikosi hicho,
Phiri alionekana kumjaribu Tambwe katika kikosi ambacho kinaweza kuanza
Jumapili huku Okwi akianza mazoezi taratibu peke yake ambapo uwezekano
wa kuwepo mechi ijayo itategemea na maendeleo ya maumivu yake.
No comments:
Post a Comment