Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri amemshauri kiungo wake
chipukizi, Jonas Mkude asiondoke ndani ya timu hiyo kwa sasa na
kumwambia akienda Yanga amekwisha.
Mkude ambaye amebakiza miezi sita kwenye mkataba
wake anahusishwa kisheria kufanya mazungumzo na hata kujiunga na Yanga
au Azam ambao wameonekana kumfuatilia kwa karibu kutokana na kiwango
chake kikubwa uwanjani.
Phiri alisema jana kuwa siyo
wakati mwafaka kwa Mkude kuondoka Simba kwani bado anahitaji
kuimarisha kipaji chake na kujikuza kiakili.
Kocha huyo ambaye ameshahakikishiwa usalama wa
ajira yake na uongozi wa klabu hiyo, alisema endepo mchezaji huyo
ataondoka kwenda Azam au Yanga, basi atakwenda kumaliza kipaji chake.
“Mimi kama kocha sikubali kumwachia mchezaji kama
Mkude kwani bado ana umuhimu na ni kijana mwenye uwezo mkubwa na kocha
yeyote angependa kuwa naye kikosini. Lakini, ninachomshauri asiwe na
haraka ya kuondoka ndani ya Simba kwani bado anatakiwa kubaki na
kuimarisha zaidi kipaji chake na kukuza akili ili hapo baadaye aweze
kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi,” alisema.
Aliongeza: “Kama akienda Yanga au Azam ataharibu kipaji chake kwani Simba ndio sehemu pekee inayowapa kipaumbele vijana.”
Katika hatua nyingine, suala la kuwajadili
wachezaji waliosimamishwa, Shaban Kisiga, Amri Kiemba na Haruna Chanongo
limewekwa kiporo baada ya Kamati ya Utendaji kuamua kwa pamoja
kulisogeza mbele na sasa wanashughulikia suala moja tu la kuhakikisha
timu yao inapata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting.
Wachezaji hao walisimamishwa kwa sababu tofauti
baada ya Simba kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons jijini Mbeya wiki mbili
zilizopita.
Kisiga alisimamishwa kwa utovu wa nidhamu kwa
madai ya kuwajibu lugha chafu viongozi wake wakati Kiemba na Chanongo
wanatuhumiwa kucheza chini ya kiwango.
Imeelezwa kuwa kamati hiyo ikiongozwa na rais wa
klabu hiyo, Evans Aveva iliamua kuachana na suala hilo baada ya
kutokamilika kwa baadhi ya mambo na hivyo kuona hakuna haja ya kuendelea
kulijadili.
No comments:
Post a Comment