Vurugu zimezuka katika kitongoji cha Ferguson, jimbo la Mossouri nchini
Marekani, baada ya Baraza la wazee katika mji huo kuamua kutomfungulia
mashtaka polisi mweupe aliyemuuwa kwa risasi kijana mmoja mweusi.
Mwendesha mashtaka wa kaunti ya St Louis Bob McCulloch alisisitiza kuwa baraza la wazee lililofanya vikao kila wiki tangu Agosti 20, ndilo “pekee lililomsikiliza kila shahidi na kupitia ushahidi wote uliokusanywa”, Baraza hilo limesema kuwa polisi mweupe Darren Wilson, alimuua Michael Brown aliyekuwa na umri wa miaka 18, kama hatua ya kujikinga na kwa hivyo hawatamfungulia mashtaka.
McCulloch alisema mashahidi wengi waliwasilisha taarifa za kutatanisha ambazo hazikuendana na ukweli wa mazingira ya tukio. Baraza hilo liliusikiliza ushahidi wa zaidi ya saa 70 kutoka kwa mashahidi 60, wakiwemo watalaamu watatu wa kimatibabu, wa damu, sumu na silaha. Katika tangazo lake, McCulloch hakutaja kuwa Brown hakuwa na silaha wakati wa kifo chake.
Wananchi wameandamana kupinga uamuzi wa baraza la wazee kutomfungulia mashtaka Afisa wa polisi Wilson
Rais wa Marekani Barack Obama na familia ya kijana Michael Brown
waliomba kuwepo utulivu baada ya tangazo hilo la majaji kutolewa. Obama
alizungumza moja kwa moja kutoka Ikulu ya White House, wakati vituo vya
televisheni vikionyesha maandamano yenye vurugu mjini Ferguson. Obama
alisema Wamarekani wanastahili kukubali uamuzi huo wa jopo la mahakama.Katika kipindi cha saa chache, majengo kadhaa yalichomwa moto na milio ya mara kwa mara ya rasasi kusikika. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi ili kujaribu kuyatawanya baadhi ya makundi ya waandamanaji.
Tukio ambalo Darren Wilson alimpiga risasi na kumuua Brown baada ya kutokea majibizano kati yao mnamo Agosti 9 yalizusha mdahalo mkali kuhusu namna polisi wanavyowatendea vijana wa Marekani wenye asili ya Afrika na kuzingatia mivutano ya muda mrefu ya ubaguzi wa rangi katika kitongoji cha Ferguson na kwingineko Marekani, ikiwa ni miongo minne baada ya vuguvugu la haki za kiraia katika miaka ya sitini.
Maelfu ya watu wameandamana kutoka Los Angeles hadi New York, huku waandamanaji katika majimbo ya Oklahoma na California wakifunga barabara. Familia ya Brown ilitoa taarifa wakisema “wamesikitishwa sana” na uamuzi wa baraza la wazee lakini wakautaka umma kuonyesha hasira zao katika njia itakayoleta mabadiliko yenye manufaa.
No comments:
Post a Comment