Saturday, 1 November 2014

Ukawa kujulikana Kisheria sasa

Ushirikiano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) siku si nyingi huenda ukatambulika kisheria baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kueleza mpango wake wa kuifanyia maboresho Sheria ya Vyama vya Siasa ili kutambua ushirikiano wa aina hiyo.
Juzi Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alieleza ugumu wa Ukawa katika kushughulikia suala la ruzuku, lakini jana Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema maboresho yanaweza kuondoa mvutano kuhusu suala la ruzuku kwa vyama vitakavyoamua kushirikiana kwa sababu ushirikiano huo utakuwa wa kisheria.
Wakati Nyahoza akieleza hayo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ruhusa ya Jaji Mutungi,  Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema moja kati ya vitu vinavyofanyiwa kazi na umoja huo kwa sasa ni kuhakikisha sheria ya vyama vya siasa inaboreshwa, ili vyama viweze kuungana na kushirikiana.
Hivi karibuni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alisema ili vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD viweze kuungana Sheria ya Vyama vya Siasa inatakiwa kurekebishwa ili kuviwezesha kusimamisha mgombea mmoja.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, vyama vya siasa vinaweza kumuunga mkono mgombea wa chama fulani lakini haviwezi kuwa na umoja utakaopewa jina kisheria, kisha kusimamisha mgombea mmoja lakini kila chama kikibaki na utambulisho wake na kusisitiza kuwa mabadiliko ya sheria hiyo aliyaacha ofisini kwake.
Jumapili iliyopita vyama hivyo vinne vilisaini makubaliano ya kushirikiana katika mambo saba, likiwamo la kusimamisha mgombea mmoja katika ngazi zote kuanzia chaguzi za serikali za mitaa hadi Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika ufafanuzi wake Nyahoza alisema, “Mchakato huu unaendelea na uko katika hatua nzuri. Wadau wametoa maoni yao kwamba ushirikiano wa vyama utambulike kisheria na kupewa usajili na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.”
Aliongeza, “Kwa hali ilivyo sasa ushirikiano wa Ukawa hautambuliki kisheria lakini pia sheria haizuii uwapo wake. Tunachotaka kukifanya ni kuongeza kipengele cha kutambua ushirikiano wa vyama katika sheria ya vyama vya siasa.”
Alifafanua kuwa kama kipengele hicho kingekuwapo, ofisi ya msajili ingetoa usajili wa ushirikiano wa Ukawa huku akitolea mfano ushirikiano wa vyama vya siasa nchini Kenya.
 “Tungekuwa na kipengele hicho katika sheria maana yake ni kwamba makubaliano ya Ukawa yangesajiliwa na msajili na hicho ndiyo kilichofanyika Kenya,” alisema.
Nchini Kenya vyama viliungana na kuzaliwa umoja uliopewa jina la Jubilee na kusimamisha mgombea mmoja na muungano huo ndio uliotoa mshindi, Rais Uhuru Kenyatta. Pia, viliungana vyama vingine na kuzaliwa umoja mwingine uliopewa jina la Cord.
“Ushirikiano ukitambulika kisheria vyama vitashirikiana katika kupata haki za pamoja ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya pamoja, hata utaratibu wa ruzuku kupitia ofisi ya msajili utakuwa mzuri maana yanakuwa ni makubaliano ya kisheria,” alisema.
 lipoulizwa lini muswada huo utawasilishwa bungeni alisema: “Bado. Hatuwezi kusema lini lakini mchakato upo katika hatua nzuri na hili tutalifanya siku za karibuni.”
Akizungumzia suala hilo Mbowe alisema, “Jambo hilo hivi sasa ndio tunalifanyia kazi. Achana na ushirikiano, kama tukitaka kuungana ni lazima tukubali kupoteza wabunge, madiwani na kila kitu. Ni lazima tuanze upya. Ndio maana nasema sheria hii ipo kwa ajili ya kuvifanya vyama vya upinzani visiungane.”
Mbowe alisema hata Katiba ya sasa haisemi chochote juu ya vyama kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyo kwa Katiba ya Zanzibar.
“Tunapenda kuungana lakini tatizo ni sheria, jambo hili ni zuri na tunaweza kulipigania likapelekwa bungeni lakini kutokana na wingi wa wabunge wa CCM wanaweza wakalipinga,” alisema.
Tendwa
Tendwa ambaye alistaafu nafasi ya Usajili wa Vyama vya Siasa Agosti mwaka jana, alisema
vyama vinavyounda Ukawa kwa sasa haviwezi kuungana na kuweka mgombea mmoja wa urais na kumuita mgombea wa Ukawa, kwani sheria haisemi hivyo.
Alisema mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hiyo aliyaacha ofisini na kwamba yanatakiwa  kwenda katika Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Kamati za Makatibu Wakuu,  Baraza la Mawaziri ambalo linaweza kutoa maelezo kwenye kamati yake ndogo ambayo inashughulikia masuala ya kisheria.
Alisema kuwa jambo hilo lilipopendekezwa wadau waliliunga mkono bila kufahamu kuwa muungano uliopendekezwa sio ule unaoweza kuvifanya vyama vya siasa kusimamisha mgombea mmoja na kuwa na jina moja.
Alisema mapendekezo hayo yalikuwa ni mapendekezo ya kuunganisha vyama (Merge) ambayo ni kuunganisha vyama na kuwa chama kimoja.
Alisema mfumo uliotakiwa upendekezwe na wadau ni muungano wa vyama (Alliance) ambao vyama vinaweza kushirikiana chini ya mwamvuli mmoja kwa kujiita jina moja, kisha kusimamisha mgombea mmoja kwa jina hilo, ila kila chama kinabaki na utambulisho wake.
Alisema hivi sasa jambo hilo linatakiwa kupigiwa debe na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili lifanyiwe marekebisho na muungano wa ‘Alliance’ ndio uingie katika sheria.

No comments: