Thursday, 27 November 2014

Waziri Mkuu atakiwa Kujiuzulu kutokana na sakata la ESCROW

Ripoti ya Kamati ya bunge ya Hesabu za Serikali imewataja baadhi ya vigogo wanaohusika na kashfa ya IPTL Nchini Tanzania akiwemo Waziri Mkuu na kuwataka kuwajibika kisiasa na kisheria.
Sakata hiyo ya IPTL inahusihswa na upotevu wa mamilioni ya fedha na kwa muda mrefu umezusha mjadala mzito katika bunge la Tanzania.
Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Zitto Kabwe na makamu mwenyekiti Deo Filikunjombe, imethibitisha kuwepo mazingira ya udanganyifu na ufisadi katika mchakato wa malipo yaliyofanyika na kueleza kuwa upotevu huo wa fedha ungeweza kudhibitiwa kama kungekuwa na uwajibikaji wa kutosha kwa baadhi ya viongozi.
Mizengo Pinda waziri mkuu wa Tanzania ametajwa kwenye ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni
Kamati hiyo imewataja viongozi wengine wanaotakiwa kuwajibika kutokana na kashfa hiyo kuwa ni mwanasheria,Waziri wa nishati na Madini, Naibu Waziri wa Nishati pamoja na viongozi wengine wa bodi.
Ripoti hiyo ilitokana na ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilianika ukiukwaji mkubwa wa taratibu wakati wa uchotaji wa fedha hizo pia mahojiano na mkurugenzi mkuu wa Takukuru na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Waziri Pinda amelimbikizwa lawama ikidaiwa kuwa alijua kuwapo kwa ufisadi huo na matamshi yake kuwa fedha hizo hazikuwa mali ya umma, wakati Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema ameonekana kutoishauri vizuri Serikali na pia kuagiza fedha hizo zitolewe kwenye akaunti hiyo.
Waziri Sospeter Muhongo amelaumiwa kwa kukosa kuchukua hatua wakati akijua kuwapo kwa sakata hilo, huku naibu wake, Stephen Masele akitiwa hatiani kwa kulidanganya Bunge.
Kashfa nyingine zilizowahi chukua uzito mkubwa katika bunge la Tanzania na kusababisha viongozi kuwajibika wakiwemo Waziri Mkuu ni pamoja na kashafa ya Richmond,EPA na sasa hii ya ESCROW ambayo kwa mara nyingine kamati hiyo imeonyesha wazi mapendekezo yake ya kutaka kuwajibika kwa waziri mkuu, Mawaziri na viongozi wengine.

No comments: