Thursday 27 November 2014

Arsenal yainyamazisha Dortmund kwenye champions league

Champions League Arsenal London vs Dortmund 26.11.2014
Magoli mawili ya kiustadi kutoka kwa Alexis Sanchez na Yaya Sanogo yaliipa Arsenal ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Dortmund. Wakati Leverkusen ikifungwa goli moja kwa sifuri na Monaco
Mjini London, wenyeji Arsenal waliutawala mchezo na kuwanyamazisha kabisa Dortmund kuanzia mwanzo: wakati Yaya Sanogo akifunga baada ya sekunde 72 tu. Lilikuwa goli la kasi zaidi kuwahi kufungwa dhidi ya Dortmund katika mchuano wa Champions League, hata kama kulikuwa na uwezekano mdogo wa mchezaji huyo kuwa katika nafasi ya kuotea.
BVB iliiruhusu Arsenal kushambulia kwa kasi ambapo Alexis Sanchez alikuwa na uhuru wa kutamba na kuuchezea mpira anavyotaka kwa ushirikiano na washambuliaji wengine wa Arsenal kama vile Alex Oxlade Chamberlain. Katika kipindi cha pili, Sanchez alifunga bao safi sana kwa kuipinda shuti yake hadi langoni kutoka nje ya eneo la hatari.
Kocha wa Dortmund Jurgen Klopp amesema baada ya mchezo kuwa “walistahili kushindwa, hata ingawa walikuwa na nafasi kadhaa za kufunga goli”. Amesema sasa lazima wawashinde Anderlecht na kisha kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye Kundi lao.
Champions League Leverkusen vs Monaco 26.11.2014Monaco waliunyamazisha uwanaja wa BayArena licha ya Leverkusen kuumiliki mpira mara nyingi
Leverkusen yabumburushwa
Mjini Leverkusen, timu yake kocha Roger Schmidt kwa mara nyingine – kama tu katika mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Monaco – iliutawala mchuano dhidi ya mpinzani wake lakini ikaambulia patupu.
Monaco walianza mchezo kwa kujikinga, kama tu ilivyotarajiwa, na kuwaruhusu Leverkusen kufanya shambulizi baada ya jingine. Ila hakuna mafanikio yaliyopatikana. Katika kipindi cha pili, mambo yalikuwa hay ohayo, hadi pale mchezaji wa zamani wa Leverkusen ambaye sasa anachezea Monaco, Dimitar Barbetov alipokimbia kwa kasi na kumwandalia pasi Nabil Dorar, ambaye naye akaandaa krosi safi katika eneo hatari ambayo ilimpaka mshambuliaji wa Argentina Lucas Ocampos aliyetikisa wavu bila kupoteza wakati.
Kwingineko Ulaya
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, mabingwa mabingwa watetezi Real Madrid walipata ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Basel, wakati makamu bingwa Atletico Madrid wakiwabumburusha Olympiakos kwa kuwazaba mabao manne kwa sifuri. Nchini Bulgaria, Liverpool walitoka sare ya mabao mawili kwa mawili na Ludogorets. Juventus, iliipiku Malmo mabao mawili kwa bila, wakati Anderlecht ikipata ushindi kama huo dhidi ya Galatasaray. Awali, Zenit St Petersburg iliishinda Benfica goli moja kwa bila.

No comments: