Friday 7 February 2014

Msichana aliyebakwa Kenya alipwa fidia

Msichana aliyebakwa na genge la watu sita nchini Kenya hatimaye huenda akapata kutendewa haki.

Liz mwenye umri wa miaka 16, alibakwa na kujeruhiwa vibaya mwezi Juni baada ya kutupwa ndani ya shimo la choo katika jimbo la Busia Magharibi wma Kenya.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na mashirika ya kutetea haki za wanawake, FIDA na COVAW kwa ushirikiano wa mwendesha mkuu wa mashitaka nchini Kenya ilisema kuwa mashauriano yanaendea kati yao hasa baada ya mkutano wao wa Februari tarehe tatu ambapo walikubaliana kuwa kesi ya Liz itaendelea mahakamani bila kucheleweshwa tena.

Wanasisitiza kuwa lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wanaodhulumiwa wanapata haki.

Inaarifiwa taarifa ya wauguzi pia inathibitisha kuwa msichana huyo alidhulumiwa kingono.

Mnamo mwezi Novemba mwaka jana mkuu wa polisi David Kimaiyo alisema kuwa huenda kesi ya Liz ikakosa kusikilizwa kutokana na kukosa ushahidi wa kutosha .

Katika taarifa yakle alisema kuwa kwa kuwa msichana huyo alichukua miezi miwili kuripoti kisa chake kwa polisi, huenda isiwezekane kuwafungulia mashitaka washukiwa bila ya ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa alibakwa.

Wanaharakati nje ya mahakama wakita Liz atendewe haki

Hata hivyo mashirika ya kutetea wanawake yalianzisha kampeini ya kutaka washukiwa sita waliombaka Liz tarehe 27 mwezi Juni 2013, baada ya kupata taarifa kuwa washukiwa hao walipewa adhabu ya kukata nyasi badala ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo mkuu wa polisi alitetea hatua ya washukiwa kuachiliwa akisema kuwa wazazi wa Liz waliafikiana na polisi kuwasamehe washukiwa baada ya Liz kukanusha kuwa alikuwa amebakwa.

Moja ya mashirika hayo COVAW ambalo hupambana na dhuluma dhidi ya wanawake, limesema kuwa litahakikisha kuwa familia ya Liz pamoja na mwathiriwa wataendelea kupata ushuri wanaohitaji na kwamba watashinikiza kesi hii kwa niaba ya Liz.

Mwendesha mkuu wa mashitka amesema kuwa atahakikisha kuwa familia ya Liz inalindwa hasa ikizingatiwa kuwa atatoa ushahidi dhidi ya watu waliombaka.

Pia uchunguzi unafanywa kuhusiana na polisi walioshughulikia kesi hiyo kwani inasemekana kuwa waliwapa adhabu ya kukata nyasi watuhumiwa kama adhabu ya kitendo chao dhidi ya Liz.

No comments: