Kikosi cha Umoja wa Mataifa kinatarajiwa kuzuru eneo ambako mauaji ya watu wengi yalifanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Hatua hii inakuja baada ya kikosi cha walinda amani cha Umoja huo nchini humo (Monusco) kugundua vijiji vitatu viliteketezwa.
Kikosi hicho kilisema kuwa zaidi ya watu hao sabini waliuawa mwishoni mwa mwezi uliopita na mapema mwezi huu.
Katika mahojiano na BBC, afisa mmoja wa shirika la Monusco, mjini Goma, Ray Tores, amesema kuwa ndege ya wanajeshi wake, iliyokuwa ikifanya uchunguzi, katika eneo hilo iligundua kuwa vijiji vitatu viliteketezwa na kuharibiwa kabisa.
Amesema kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa watazuru eneo hilo baadaye hii leo ili kufanya uchunguzi zaidi.
Jeshi la kutunza amani la Umoja wa Mataifa limeimarisha juhudi zake katika eneo hilo, hasa tangu lilipolisambaratisha kundi la waasi wa M23, Novemba mwaka uliopita.
Bwana Torres, amesema kuwa zaidi ya makundi arubaini ya waasi yanajulikana kuendesha operesheni zao katika eneo hio la Goma.
Manne kati yao yamekuwa yakifanya mashambulio ya mara kwa mara na hivyo kuwa tishio kubwa la usalama.
Umoja wa Mataifa, umesema kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na makundi ya waasi yaliyojihami katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ili kuwatia hofu watu wanaoishi katika eneo hilo.
Afisa huyo amesema kuwa wengi wa waliouawa walikuwa na majeraha ya mapanga.
No comments:
Post a Comment