HALI ya afya ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 12, mwanafunzi wa darasa la nne, shule ya msingi Bwanza, kata ya Kisorya, wilaya ya Bunda mkoani Mara, aliyeingiwa na samaki sehemu zake za siri na kukimbilia tumboni inazidi kuimarika.
Mtoto huyo ametoa ushuhuda wa tukio hilo akisema hatalisahau kamwe maishani mwake.
"Nilikuwa nateka maji ziwani, samaki huyo aina ya sato akarukia miguuni mwangu, akaingia sehemu za siri na kukimbilia tumboni, nilijaribu kumvuta lakini sikufanikiwa, kwani alizama kabisa tumboni kupitia sehemu zangu za siri," alisema mtoto huyo ambaye jina lake tunalihifadhi.
Mtoto huyo anayetibiwa kwa mganga wa jadi aliyejitambulisha kwa jina moja la Mshaki alisema, samaki huyo alipomuingia sehemu zake za siri, alisikia maumivu makali na kushangaa namna samaki huyo alivyokua akiteleza kuingia tumboni.
Alisema kila alipokuwa akijaribu kumvuta ili amtoe, alihisi maumivu makali zaidi hivyo akalazimika kumwacha na kuingia tumboni.
"Samaki alipoingia huku chini miguuni na kukimbilia tumboni, niliishiwa nguvu, nilimuita dada Monica niliyekuwa naye ziwani akanisaidia kunishika hadi nyumbani, usiku sikulala, tumbo lilikuwa likiniuma mno, kila nilipojisaidia haja ndogo nilikuwa nikijichungulia na kuona mkia wa samaki huyo ukitokea, hata bibi Emakulata naye alimwona aliponichungulia," alisema mtoto huyo.
Alisema kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kutibiwa na mganga huyo wa kienyeji mkazi wa kijiji cha Amuyebe, Ukerewe mkoani Mwanza japo alisema baada ya kupewa dawa, alitokwa na harufu mbaya.
Aidha, mganga huyo wa jadi, akizungumza na Majira kwa njia ya simu. alikiri kumtibu mtoto huyo akidai alichezewa kichawi kwa kuingiziwa dawa tumboni kupitia sehemu zake za siri kwa mwonekano wa samaki, dawa ambayo alisema, ilikuwa iozeshe viungo vyote tumboni na kumsababishia kifo.
"Mtoto huyu alirushiwa kombora katika mwonekano wa samaki aliyeingia tumboni mwake kupitia sehemu zake za siri, lengo likiwa ni kumuua baada ya kuozesha viungo vyote tumboni lakini, nimemwahi kabla hajaharibu tumbo lake kwa kumpa dawa ya kumfanya aharishe na kukojoa mara kwa mara, ndiyo maana alitokwa na harufu mbaya.
Bibi wa mtoto huyo, Emakulata Mtani (64), alisema ana furaha kubwa kutokana na maendeleo mazuri ya afya ya mjukuu wake akiamini kwa hali ilivyo sasa atapona.
Januari mosi, mwaka huu mtoto huyo akiwa anateka maji katika Ziwa Victoria kumwagilia bustani ya nyanya na vitunguu, alidai kurukiwa na samaki aina ya sato sehemu zake za siri, aliyepenya hadi tumboni mwake.
Miongoni mwa viongozi waliozungumza na Majira na kuthibitisha kupata taarifa za kutokea kwa tukio hilo la aina yake ni mwenyekiti wa kitongoji cha Alwego Leticia Bituro, Diwani wa kata ya Napindi Elias Magoti, Kamanda wa Jeshi la Polisi wilaya ya Bunda (OCD) Mika Nyange.
No comments:
Post a Comment