Thursday, 13 February 2014

Wafanyakazi wa Red Cross watekwa Mali

Kundi la wapiganaji la MUJAO nchini Mali

Shirika la habari la AFP linasema kuwa kundi la wafanyikazi wa shirika la msalaba mwekundu ambao walitoweka Kaskazini mwa Mali limetekwa nyara na wapiganaji wa kiislamu.

Shirika hilo linasema kuwa wapiganaji wa kundi la umoja na Jihad Magharibi mwa Afrika (Mujao) wamethibitisha kuyakamata magari manne na kusema kuwa abiria waliokuwa ndani ni maafisa wa shirika la msalaba mwekundu.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya kati , Generali Babacar Gaye, ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za dharura kuzuia kuenea kwa ghasia zaidi ambazo anasema zinaligawanya taifa hilo .

Wafanyakazi wa shirika hilo wanasema kuwa waliotekwa nyara wako salama na bukheri wa afya mikononi mwa wapiganaji hao wa kiislamu.

Kundi la MUJAO ni moja ya makundi ya wapiganaji walio na uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda ambalo lilidhibiti kaskazini mwa Mali mwaka 2012 kabla ya kuondoshwa kutoka eneo hilo na wanajeshi wa Ufaransa mwezi Januari mwaka jana.

Kundi hilo linasemekana kutuma taarifa iliyosema, ''Asante kwa Mungu tumekamata gari lenye maadui wa uisilamu wakiwa na washirika wao. ''

Msemaji wa shirika hilo Alexis Heeb kulingana na AFP alisema kuwa wafanyakazi hao wanne wa shirika la Red Cross na mfanyakazi mmoja kutoka katika shirika lengine la misaada walitoweka Jumamosi wakiwa ndani ya gari lao katika eneo lililo kati mwa miji ya Kidal na Gao.

Watu hao wote ni raia wa Mali.

AFP ilimnukuu msemaji huyo akisema kuwa'' sasa hivi tuna wasiwasi mkubwa na tunajaribu kuwasiliana na kila mtu tunayemjua kuhakikisha usalama wao. Inaarifiwa kuwa kundi hilo linarejea katika ngome yao mjini Gao.

No comments: