Tuesday 11 February 2014

Kimbunga chavuruga makazi, na miundo mbinu

Upepo mkali uliovuma mithili ya kimbunga, umeezua mapaa ya nyumba zipatazo 200 katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro na kusababisha mamia ya familia, kokosa mahali pa kuishi.

Maafa hayo yametokea wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikiwa imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua na upepo mkali katika maeneo mbalimbali kuanzia leo hadi keshokutwa.

Katika Mkoa wa Morogoro, nyumba 183 zimeezuliwa kutokana na upepo mkali uliojitokeza jana katika Kata za Kidatu Sanje, Mkamba na Mkula, wilayani Kilombero.

Upepo huo uliodumu kwa takriban saa mbili, pia umeharibu mazao na kuangusha miti ambayo mingine iliangukia kwenye nyumba na kuzibomoa.

Taarifa kutoka katika maeneo hayo zilibainisha kuwepo kwa majeruhi mmoja aliyeangukiwa na mti, lakini aliwahishwa katika Hospitali ya Mtakatifu Francis, mjini Ifakara kwa matibabu.

Kwa mujibu wa habari hizo, watu waliokosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa, wamepata hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, David Ligazio, alikiri kuwa upepo uliovuma katika maeneo hayo, haujawahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 iliyopita.

“Ni kweli kumetokea upepo mkali uliodumu kwa muda wa saa mbili na baadhi ya nyumba za watu zimeathirika, watu wanaishi kwa ndugu na jamaa zao. Kwa sasa tunaangalia namna ya kusaidia,” alisema mwenyekiti huyo.

Katika maeneo ya Shule ya Msingi Itefa, kulibainika kuwa vyumba vinne vya madarasa na viwili vya ofisi za walimu vimeezuliwa kwa upepo huo ulioanza wakati tayari wanafunzi wakiwa wameruhusiwa kurudi nyumbani.

Tofauti na ilivyotokea Kilombero, katika Wilaya ya Same, upepo huo uliandamana na mvua kubwa yaliyosababisha mapaa ya nyumba kuezuliwa na Barabara ya Dar es Salaam – Moshi eneo la Hedaru kufungwa kwa muda.

Katika Kata ya Makanya, zaidi ya nyumba nane zimeezuliwa na nyingine kuanguka.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, alisema maafa hayo yametokana na mvua zilizoanza kunyesha tangu juzi na kusababisha maji kutoka maeneo ya milimani kufurika katika uwanda wa chini ambao ni tambarare.
“Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya milimani zimesababisha maji kujaa katika maeneo ya tambarare. Nyumba zimejaa maji, pia imeathiri ujenzi wa madaraja katika Barabara ya Same –Mombo,” alisema.

Kujaa kwa maji katika barabara hiyo, kumesababisha msururu mkubwa wa magari yaliyokuwa yakitoka Arusha kwenda Dar es Salaam na Tanga.

Pia yaliyotokea Moshi Kilimanjaro na Arusha kwenda katika majiji ya ya Dar es Salaam na Tanga.

No comments: