Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ametaka mabango yanayoonyeshwa na wananchi kwa
viongozi wa kitaifa wanapowatembelea yasiwe yanazuiwa kwa vile yanakuwa
yanaelezea changamoto wanazokabiliana nazo.
Majaliwa alisema hayo baada ya kuona mabango yaliyoinuliwa na wananchi
kwenye mkutano wake na wananchi mwishoni mwa juma lililopita mjini
Sikonge mkoani Tabora huku wananchi hao wakitakiwa kuyashusha.
“Siku nyingine msirudie na kuanzia sasa waacheni wananchi waonyeshe
mabango yao kwani ndiyo njia wanayotumia kuonyesha hisia zao kwa yale
wanayokumbana nayo na kuwasababishia kero,” alisema Majaliwa.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu aliwaagiza wasaidizi wake wayakusanye
mabango yote wayaandike kisha wampelekee yaliyomo akiahidi kwamba
atayafanyia kazi.
Alieleza kuwa malalamiko mengi kwenye mabango hayo yanahusu kero za
vyama vya msingi vya ushirika na migogoro ya ardhi na kumtaka Mkuu wa
Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kutenga siku kwa ajili ya kusikiliza kero
za wananchi huku akiwa na wakuu wa idara mbalimbali.
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa wananchi kuinua mabango kwa viongozi wa
kitaifa. Julai 22 huko Kigoma wakati wa ziara ya Rais John Magufuli,
wananchi waliinua mabango yao ili ayasome huku wakizuiwa na walinzi.
“Waacheni, waacheni tu jamani…jamani mtulie nitayasoma yote. Nimeyaona
yote ndiyo maana nayapitia na wasaidizi wangu wanayapiga picha nyinyi
msiwe na wasiwasi,” alisema Rais Magufuli wakati akihutubia katika
Uwanja wa Lake Tanganyika huku wananchi wakikazana kumwonyesha mabango
yao.
Hali kama hiyo ilijitokeza tena huko Tabora Julai 23, wakati Rais
Magufuli akiwahutubia wananchi na kuwataka washushe mabango yao kwa
sababu wananchi walikuwa wakipiga kelele, jambo lililokatisha hotuba
yake.
“Naomba myashushe mabango yenu ili niendelee na hotuba yangu,” alisema
Rais Magufuli lakini wananchi waliendelea kuyainua juu, jambo
lililoonyesha kumkera, “Nimesema shusheni hayo mabango, la sivyo
siyashughulikii. Ukitaka hata ukayatandike kwenye kitanda cha mke wako,
siyasomi.”
Akitoa maoni yake kuhusu vitendo vya wananchi kuinua mabango yao kwa
viongozi wa kitaifa, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Benson Bana alisema hiyo inaonyesha kukua kwa demokrasia nchini.
Alisema wananchi wanatafuta namna ya kufikisha ujumbe kwa viongozi wa
kitaifa juu ya mambo ambayo Serikali za mitaa au mkoa zimeshindwa
kukabilaiana nazo au wameshindwa namna ya kuwafikia.
“Huko ndiko kupevuka kwenyewe na kukua kwa demokrasia. Viongozi kwenye
maeneo hayo wameshindwa kutatua kero za wananchi ndiyo maana wananchi
wanaona bora watumie fursa ya kueleza kero zao kupitia mabango,”
alisema.
Mwanazuoni huyo alisisitiza kwamba kuna haja ya kuimarisha mifumo ya
mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao wa Serikali za mitaa mpaka
mkoa ili kumaliza changamoto zao bila kuzifikisha kwa viongozi wa
kitaifa.
“Viongozi wa mikoa wawe na mawasiliano ya karibu na wananchi, wawe
wanajibu meseji zao na kuwafikia katika maeneo yao. Hiyo itasaidia
kupunguza mabango kwa viongozi, japo siyo jambo baya pia kuinua
mabango,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kitendo
cha wananchi kuonyesha mabango kwa viongozi kinaonyesha udhaifu wa
Serikali katika kukabiliana na changamoto za jamii husika.
Alisema mara nyingi askari wamekuwa wakiwazuia wananchi kupaza sauti zao
ndiyo maana nao wameamua kuja na mtindo wa kutumia mabango kufikisha
ujumbe kwa viongozi wao wa kitaifa. “Katiba yetu inaruhusu uhuru wa
kutoa maoni bila kujali kwamba yatawafurahisha au kuwakera viongozi.
Askari wasitumie nguvu kuwanyamazisha wananchi kwa sababu ni haki yao ya
msingi,” alisema Muabhi.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) alimpongeza
Waziri Mkuu kwa kutambua umuhimu wa sauti ya umma na kusisitiza kwamba
hiyo ni njia moja wapo ya kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Alisema siyo jambo baya kwa wananchi kuinua mabango yao kwa viongozi kwa
sababu wakati mwingine wanawakumbusha juu ya mambo ambayo wanatakiwa
kuyafanyia kaz
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment