Friday, 21 July 2017

Mawakili Kigali walaani kukamatwa Rais wa wanasheria Tanganyika, Tundu Lissu

Baadhi ya Mawakili jijini Kigali wamekosoa kitendo cha Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam cha kumkamata rais wa chama cha wanasheria Tundu Lissu ambaye alikuwa njiani kuelekea jijini humo kuhudhuria mkutano.
Tundu Lissu ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), amekamatwa leo, Alhamisi, Julai 20 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)  akielekea Kigali, Rwanda  kwenye kikao cha Halmashauri ya EALS kinachoanza kesho.
”Huu ni mpango wa kumdhoofisha, kwanini asingekamatwa jana?” amehoji wakili wa kujitegemea Rwebangiza Kiondo kutoka Tanzania, ambaye yupo jijini humo kwa shughuli za kufuatilia uchaguzi wa Rwanda.
Wakili Rwebangiza ameiambia BBC, kuwa Polisi wanatumia nguvu nyingi kupambana na Mwanasheria huyo ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake.
”Unamkamata Wakili akiwa katika pilika za kutekeleza wajibu wake, tena kwa kumshtukiza utafikiri ni jambazi anayetafuta, sikatai kwamba huenda pana hoja lakini kwanini umshtukize, mtu ambaye ni mbunge?”

Wakili mwingine ambaye hakutaka kuandikwa jina lake hadharani amesema kuwa Polisi haijaonesha weledi kwa kumkamata mtu ambaye hakuwa na kosa la Jinai.
”Wakati anagombea urais wa TLS(Chama cha Mawakili Tanganyika) walimvizia wamkamate lakini baadaye alikamatwa na kuachiwa,binafsi naona huu ni uonevu na mwendelezo wa kuizoofisha taaluma ya Mawakili” amesema Wakili huyo.
Wakili Msemo Aljebra anasema Tundu Lissu alikuwa kesho Julai 21 awasilishe mada ambayo ni muhimu katika mkutano huo.
”Siyo kila wakati nguvu inatumika, kwa hili busara ilipaswa kutumika zaidi, na kumuachia kiongozi huyo, binafsi sikuona sababu ya kumvizia, na ilihali alipaswa kuwasilisha mada kesho” amesema Msemo.
Wakili wa CHADEMA, Peter Kibatala amesema jioni hii kuwa, kama Polisi wamemkamata Lissu, wakamilishe taratibu zao wampeleke mahakamani ili wakutane huko.

No comments: