Kauli ya Rais John Magufuli kwamba yuko tayari kuutoa mwili wake
sadaka katika kupambana na rushwa na ufisadi uku kuwasaidia wanyonge,
imeibua mjadala huku wanasiasa wakitofautiana.
Akizungumza
katika Mkutano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi hivi karibuni jijini
Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema: “Unapoona watu wanashangaashangaa
sana (ni) kwa sababu hawakuzoea haya. Na walifikiri nitakuwa part of
them (sehemu yao), never (haitatokea), not me (si mimi).
“Ni
mara 10 nisiwe rais, nikachunge hata ndege, nikakae kijijini kuliko niwe
Rais halafu nivumilie uozo huu unaofanyika. I’m saying never (nasema
haitatokea).”
Rais Magufuli amekuwa akizitoa kauli kama hizo
mara kwa mara, hasa anapowawajibisha baadhi ya watendaji wa Serikali,
huku ikidaiwa kuna upinzani mkali ndani ya chama chake cha CCM, hali
inayohisiwa kusababisha kauli hiyo.
Mkurugenzi wa Fordia,
Bubelwa Kaiza alisema kauli hizo za Rais Magufuli zinaonyesha uzalendo
wa kweli na amefanikiwa kufanya mambo yaliyowashinda marais
waliomtangulia.
“Ndani ya CCM kuna upinzani mkali kutoka kwa
makada. Kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita watendaji wa Serikali wamekuwa
na mikakati ya kusaidia wezi na utapeli, hivyo anachofanya ni ‘revival
strategy (mkakati wa kufufua),” alisema Kaiza.