Thursday 29 September 2016

Raia wa Uganda Alfred Olango auawa na polisi Marekani

El CajonPolisi wamekiri kwamba Olango hakuwa na silaha
Polisi katika jimbo la California, Marekani wanasema wamemuua kwa kumpiga risasi mkimbizi wa Uganda ambaye wanasema alitoa kifaa chenye ncha kali mfukoni na kuwalekezea maafisa "kana kwamba alikuwa anawafyatulia risasi."
Baadaye, imebainika kwamba ilikuwa ni sigara ya kisasa ifahamikayo kama 'e-cigarette'.
Waandamanaji kadha wamejitokeza katika barabara za El Cajon, viungani mwa mji wa San Diego, kulalamikia kuuawa kwa Alfred Okwera Olanfo, aliyekuwa na umri wa miaka 38.
Bw Olango aliuawa Jumanne baada ya polisi kujibu wito kutoka kwa dadake Olanfo ambaye aliitisha msaada.

Aliwaambia maafisa wa polisi kwamba kakake alikuwa anaugua ugonjwa wa kiakili.
Mkuu wa polisi wa El Cajon Jeff Davis amesema Bw Olango alifariki baada ya kupigwa risasi na afisa mmoja. Polisi mwenzake alifyatua risasi za mipira za kumtuliza.
Polisi wamekiri kwamba kifaa alichokuwa nacho hakikuwa silaha.
Badala yake, wamesema alikuwa na sigara ya rangi ya fedha ya urefu wa inchi tatu (7.6cm).
Agnes Hassan, rafiki wa familia ya Bw Olango, anasema alimfahamu mwanamume huyo, ambaye anasema alikuwa na elimu nzuri lakini alikuwa na matatizo ya kiakili.
Bi Hassan anasema alikaa na Olango kwa muda katika kambi ya wakimbizi wakielekea Marekani.

Mtaa wa El Cajon, San Diego huishi watu karibu 100,000 na una idadi kubwa ya wakimbizi, wengi ambao walikimbia vita Iraq na Syria.

No comments: