Monday, 1 September 2014

Kocha wa simba ashangazwa na usajili wa Okwi



phiri
USAJILI wa straika Emmanuel Okwi ndani ya Simba, umemshtua kocha Patrick Phiri ambaye amesema haelewi nini kimetokea na sasa amewaachia viongozi waamue nani anafaa kuachwa ama kuendelea.
Juzi Alhamis jioni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe, alimtangaza rasmi Okwi kuwa mchezaji mpya wa Simba kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Mpaka jana Ijumaa mchana Okwi alikuwa hajajiunga na kambi hiyo iliyopo visiwani hapa huku kukiwepo taarifa kuwa angewasili muda wowote na taarifa za ndani zilisema kuwa beki Mkenya Donald Mosoti ndiye aliyekuwa kwenye mpango wa kuachwa.
Simba ilipitisha majina ya wachezaji 28 wakiwemo wachezaji watano wa kigeni ambao ni washambuliaji Amissi Tambwe, Raphael Kiongera, Pierre Kwizera, Joseph Owino na Mosoti.
“Bado nipo gizani, nimesikia taarifa hizo lakini nasubiri taarifa ya viongozi, naamini uongozi wa Simba upo vizuri katika kusajili hivyo mchezaji nitakayeletewa atakuwa mzuri maana wao wamemuona na amewahi kuichezea Simba,” alisema Phiri.
“Soka la Tanzania ni kama siasa hivyo tunatakiwa kukubaliana na hali halisi, mimi ni mtaalamu wa benchi la ufundi lakini viongozi pia wana utaalamu wao, hivyo naamini usajili wao utakuwa mzuri.”
Kuhusu taarifa za kutemwa kati ya wachezaji wake Mosoti au Tambwe, Phiri alisema: “Mosoti sikumpa nafasi sana ya kucheza mechi hizo kwa sababu wengi wanamfahamu na Butoyi Hussein amekuja kwa ajili ya majaribio hivyo ilikuwa ni lazima apewe nafasi ili aonyeshe kiwango chake.
“Tambwe ni mchezaji mzuri na ndiye mfungaji bora wa ligi msimu uliopita, binafsi alicheza vizuri pamoja na Said Ndemla katika mechi zilizopita, nikiwa kama kocha siwezi kusema mchezaji ameshuka kiwango kwa mechi za kirafiki.”

No comments: