Bunge la Jamhuri ya Muungano jana liliweka kando tofauti zao za
kisiasa wakati lilipowaweka kwenye kibano mawaziri watano kutokana na
utendaji wao.
Wabunge wa chama tawala na upinzani walionyesha
makali yao wakijadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha
2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka
ujao, ikiwa ni mwaka mmoja tangu Serikali ya Rais John Magufuli iingie
madarakani.
Mbali na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango, mawaziri wengine waliowekwa kwenye hali ngumu ni Ummy Mwalimu,
ambaye ni Waziri wa Afya, Angellah Kairuki (Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-Utumishi), Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na Uwezeshaji) na
Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia)
Mwongozo huo wa mpango wa kuandaa bajeti unaonyesha Serikali itatumia
Sh32.9 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha, ikiwa ni ongezeko la Sh3.4
trilioni kulinganisha na bajeti ya mwaka huu.
Mjadala wa wabunge
hao ulijielekeza katika kuchambua utendaji wa mawaziri hao na hali
ilivyo kwenye wizara zao, hasa kiuchumi ambayo inaelezwa kuwa ngumu
kutokana na wananchi kudai fedha zimepotea kwenye mzunguko.
Aliyefungua mashambulizi hayo ni mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael
Chegeni aliyesema Dk Mpango ni msomi, lakini ana “kiburi, si msikivu na
hataki kushauriwa”.
Dk Chegeni alisema wabunge walimshauri mambo
mengi waziri huyo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17,
lakini hakutaka kusikiliza na ndiyo maana hali imekuwa ngumu kila eneo.
‘’Dk Mpango unapaswa kuwa msikivu na kuacha kiburi.
Tunayokushauri yachukue (kwa kuwa) tunakusaidia ufanye kazi.Tulikuambia
mambo mengi, ukatudharau sasa yanatokea, kila kona hakuna unafuu,’’
alisema.
Dk Chegeni alisema uchumi ambao anauzungumziwa kwenye
mpango wake hauendani na hali halisi ya maisha ya wananchi, akisema hata
halmashauri hazijapewa fedha hadi sasa.
“Wananchi hawana fedha,
wabunge hawana fedha. Fedha ambazo Mamlaka ya Mapato (TRA) inaeleza
kuwa inakusanya, ziko wapi wakati madeni yameongezeka?”
Alimtaka waziri huyo kutimiza wajibu wake kwa unyenyekevu na kwa kusikiliza ushauri wa wabunge kuhusu wizara yake.
“Umekuwa ni tatizo sana. Hata ukiitwa na jumuiya za wafanyabiashara
huendi, ukiitwa na kamati ya Bunge ya Bajeti huendi.Umekuwa mgumu
kupatikana, dhamana uliyopewa ni kubwa, usitumie vibaya mamlaka yako,”
alisema Dk Chegeni.
Mbunge mwingine aliyechangia alikuwa John
Heche (Tarime Vijijini-Chadema), ambaye alisema mtu wa pili kutumbuliwa
na Rais John Magufuli baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga atakuwa Dk Mpango.
“Kwa sababu gani utakuwa ni
wa pili kutumbuliwa? Kwa sababu mambo yanapokwama, mipango yote
mliyopanga inapokwama, wewe ndiye unabebeshwa zigo hilo ili yeye
aonekane yuko sawa wakati mnakosea wote,” alisema.
Heche alisema
wamesimamisha ajira kutafuta watumishi hewa kwa mwaka mzima, lakini
wako vijana waliosomeshwa na baba zao wako mitaani kwa kukosa ajira.
“Dada zetu wanajiuza, mikopo nayo hakuna, mnatafuta wanafunzi hewa.
Kilimo nako mnatafuta wakulima hewa. Cha msingi mseme kuwa Serikali yenu
imefilisika na hamuwezi kutekeleza kitu chochote, msaidiwe,” alisema.
Mbunge wa Solwa (CCM), Ahmed Salum aliwataka wabunge wa CCM kumwambia
ukweli Dk Mpango kuwa wanakwenda kugonga mwamba katika uchumi.
“Unajiuliza fedha zimekwenda wapi? Unakuja hapa unasema kuwa uchumi
umekua, how (kwa vipi)? Twiga imeshakuwa taken over (imeshachukuliwa),
CRDB imetangaza hasara na TIB hasara,” alisema.
Alisema hali
hiyo inaonyesha kuwa baada ya miaka miwili benki hizo zinakwenda
kufungwa na huo utakuwa ni mgogoro wa kiuchumi nchini.
Alisema
hilo huenda linatokana na mawaziri kutokwenda kuomba kura na hivyo
hawafahamu joto la maisha lililopo kwa wananchi majimboni.
“Mimi
natoka Jimbo la Solwa, unaahidi, unadanganya hadi unachoka. Alikuwa JK
ameondoka, anakuja Magufuli ataondoka hakuna lililofanyika,” alisema.
Aliitaka Serikali kurejesha fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii
ilizoziweka “kabatini” Benki Kuu na mifuko hiyo iziweke fedha hizo
kwenye benki za biashara ili fedha zianze kuzunguka.
Aliitaka
Serikali kulipa madeni ya ndani ili fedha zianze kuzunguka na kwamba
kumekuwa na joto hata ndani ya Bunge, akisema kuna ukata.
Salum
alisema makusanyo ya kodi yanayotangazwa na kuonekana kuwa makubwa
yanatokana na watu kulipa madeni ya nyuma na mara baada ya kuisha kwa
malimbikizo hayo, makusanyo yatabaki kama ilivyokuwa wakati wa Serikali
ya Awamu ya Nne.
“Watalipa itafika mahali itakwisha na kubaki na
makusanyo ya siku hiyo, cash revenue (fedha taslimu). Hapo ndipo
itashuka kutoka Sh1.5 trilioni hadi Sh800 bilioni iliyoachwa na Rais
Jakaya Kikwete,” alisema.
“Haya madeni yakiisha tutarudi
kukusanya bilioni. Hatuwezi kufika trilioni hizo za leo. Tuna matatizo.
Kipindi cha Kikwete, TRA ilikuwa inakusanya Sh850 bilioni, lakini nchi
ilikuwa nzuri na mambo mengi yalienda vizuri kuliko sasa.”
Alisema Rais Magufuli amekuwa na maono mazuri ya kuifanya nchi kufikia
mafanikio ya Thailand, lakini tatizo wasaidizi wake hawamwambii ukweli
ama wanaogopa kufukuzwa.
“Magufuli tulikuwa naye hapa kwa zaidi
ya miaka 10, namfahamu. Ukienda na data (takwimu) ukamueleza kukimbiwa
na wafanyabiashara bandarini, atakuelewa,” alisema.
Mbunge wa
Nzega Mjini (CCM), Hussen Bashe alisema mipango ya Dk Mpango haifanani
na ahadi walizozitoa kwa wananchi kuwa watawaboreshea hali ya uchumi
watakapowachagua.
“Kwa sababu kaka yangu (Dk Mpango) hujaenda kuomba kura? Dunia imebadilika tunaenda kufa tunapaswa kubadilika,” alisema Bashe.
Alisema miradi mingine kama wa chuma wa Liganga na makaa ya mawe wa
Mchuchuma ameanza kuisikia muda mrefu, lakini hajaona utekelezaji.
Bashe alisema Waziri Dk Mpango anazungumzia bajeti ya Sh33 trilioni na
kwamba eneo la kwanza ni makusanyo ya kodi kuongezeka kwa asilimia 16,
wakati siyo mazuri.
Alisema wabunge waliwahi kuwaambia wasiweke kodi kwenye uhamishaji wa fedha, utalii na maeneo mengine, lakini hawakuwasikia.
Ndalichako
Wakizungumzia hali ya elimu, wabunge walimkosoa Waziri Ndalichako
kutokana na hali inavyoendelea, hasa suala la mikopo ya wanafunzi wa
vyuo vya elimu ya juu.
Akichangia eneo hilo, Heche alianza kwa
kukosoa kitendo cha Profesa Ndalichako kwenda kupiga kura katika
uchaguzi wa meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni uliofanyika
wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam.
“Leo elimu ni
majanga. Mimi nilikuwa nakuheshimu sana Profesa Ndalichako ukiwa Katibu
wa Baraza (la Mitihani la TaifaNecta). Umewahi kuonyesha watu wamechora
mazombi kwenye mitihani,” alisema.
“Wewe umepewa wizara hii,
umechora Zombie kubwa kuliko wale waliochora kwenye mitihani, sijui hata
wizi wa mitihani utazuiaje kama wewe Profesa ulitoka hapa kwenda kuiba
kura Kinondoni.”
Alisema hivi sasa Bunge wamelifanya kama idara fulani ya Ikulu inayohusika na umwagiliaji maji katika maua.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Wataira alisema Ndalichako alipiga
kura za kuwachagua mameya wa halmashauri za manispaa za Kinondoni na
Ilala.
“Ulikuwapo juzi kwenye uchaguzi wa meya Kinondoni wakati
ulishapiga kura katika umeya wa Ilala, Profesa mzima unahusika katika
wizi wa kura,” alisema.
Mwijage
Pia Waziri Mwijage alikuwa
kwe- nye kikaangio hicho. Akichangia suala la mpango wa Serikali
kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda, Dk Chegeni alisema Mwijage ni
“mzee wa sound” ambaye anafanya porojo.
“Waziri wetu anajulikana
kama mzee wa porojo, sijui hiyo Tanzania ya viwanda tutafika lini.
Acheni maneno maneno na kusigana wenyewe kwa wenyewe. Mnatofautiana
kauli, kila mmoja anaongea lake. Fanyeni kazi kwa pamoja kila wizara
itoe maoni yake katika huo Mpango,” alisema Dk Chegeni.
Naye
Heche alisema hata kwa Watanzania wanamjua Mwijage kwa jina la “Mzee wa
Sound”. “Ukikutana naye hapo nje ukamsimamisha waziri, anauliza ‘vipi
unataka nikupe kiwanda’ na kutoa mkono mfukoni.
Anataka kuchomoa kiwanda mfukoni? Mpango wenu hamjajenga kiwanda hata kimoja,” alisema.
Alisema kiwanda ndicho kitaajiri watu wengi wakiwemo mamantilie,
wahasibu wahandisi na wengine wengi, lakini hadi sasa hakuna kiwanda
hata kimoja.
Kairuki
Akizungumzia suala la watumishi hewa,
mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo) Zitto Kabwe alionyesha
kushangazwa na kitendo cha mawaziri kutoa taarifa zinazotofautiana.
“Monthly Economic Review (taarifa ya uchumi ya mwezi) ya Agosti 2015
inaonyesha kwamba wages and salaries (mishahara) ambazo Serikali ililipa
Juni mwaka 2015 zilikuwa Sh456 bilioni.
"Monthly Economic
Review ya Agosti 2016 inaonyesha kwamba wages and salaries ambazo
Serikali imelipa kwa mwezi Juni 2016 ni Sh534 bilioni,” alisema Zitto.
“Kwamba kuna nyongeza ya gharama za mishahara ya kila mwezi ya Sh78
bilioni. Waziri wa Utumishi jana ameeleza wanaokoa Sh19 bilioni kila
mwezi kwa kuondoa watumishi hewa. Taarifa ya Benki Kuu inaonyesha kuwa
tangu Serikali hii iingie madarakani, gharama za watumishi kwa mwezi
zimeongezeka kwa Sh78 bilioni.”
Zito alisema pamoja na watumishi
hewa kuondolewa, ajira mpya kuzuiwa na nyongeza ya mishahara
kusimamishwa, gharama za mishahara zimeongezeka kwa Sh78 bilioni.
“Haiekeweki.
Kuna mmojawapo kati ya hawa wawili (Waziri Kairuki
na BOT) anadanganya umma. Ama zoezi la watumishi hewa ni publicity stunt
(la kujitafutia umaarufu) au Serikali inatumia fedha kwa matumizi
mengine, halafu BOT inasema ni mishahara,”alisema Zitto.
No comments:
Post a Comment