Thursday, 9 January 2014

PROFESA ANNA TIBAIJUKA AZOMEWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kapunga Rice Project Limited, Justin Vermaak akizungumza na Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Prof Anna Tibaijuka, alipotembelea shamba hilililopo Wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya juzi


Mbeya.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alipata wakati mgumu juzi jioni baada ya kuzomewa na wananchi waliokerwa na kitendo chake cha kubadilika na kumruhusu mwekezaji kuendelea kumiliki eneo la ardhi katika Shamba la Kapunga, Wilaya ya Mbarali, Mbeya.

Ilibidi Mkuu wa Wilaya hiyo, Gulam Hussein Kifu aingilie kati kuwatuliza wananchi hao waliokuwa wakipiga kelele na kutoa maneno makali kwa waziri huyo.

Profesa Tibaijuka alikwenda huko kwa nia ya kusuluhisha mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji wa Kampuni ya Kapunga Rice Project. Awali, shamba hilo lilikuwa mali ya Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco).

Wananchi hao walikasirishwa na hatua yake ya kuamua kuwa eneo hilo ni halali kwa mwekezaji huyo tofauti na msimamo wake wa awali wa kutaka ardhi hiyo irudishwe kwa wananchi.

Profesa Tibaijuka alibadili mawazo yake baada ya kufanya mazungumzo na mwekezaji huyo ndani ya gari akiwa na Mkuu wa Wilaya.



Msimamo awali

Profesa Tibaijuka alifika Kijiji cha Kapunga saa 6.45 mchana na kuanza kikao cha ndani na viongozi wa kijiji kwenye ofisi yao hadi saa 8.14 mchana. Alielezwa alielezwa kwamba mgogoro huo unatokana na kitendo vya mwekezaji huyo kutaka kupora ardhi yote ya kijiji chenye wakazi wapatao 4,400.

Mwenyekiti wa Kijiji, John Nyoni alisema mwaka 1995, wanakijiji walitoa hekta 5,500 za ardhi kwa Nafco ambazo ziko kwenye mradi maalumu wa kuendelea kilimo cha mpunga, lakini wanachoshangaa ni kuona aliyerithi eneo hilo (mwekezaji) anadai hekta nyingine 1,870 kutoka kwenye mashamba ya wananchi pamoja na kijiji chote.

Nyoni alidai kuwa katika harakati hizo, mwekezaji huyo alipokonya shule, zahanati ya kijiji na sasa anataka kuwaondoa wananchi wote. Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Tibaijuka alisema alifika hapo kutoa jawabu la suluhisho na kwamba atakachotoa ni cha mwisho wala hakutakuwa na mgogoro mwingine tena.

“Serikali imetambua chanzo cha makosa ni Nafco kusajili na kupata hati moja kwa eneo lote likiwamo la kijiji pamoja, hivyo mwekezaji huyo alikabidhiwa hati hiyo ikionyesha eneo la hekta 7,370 badala ya hekta 5,500,’’ alisema Profesa Tibaijuka.

Aliwahakikishia viongozi wa kijiji hicho chenye vitongoji saba kwamba alifika hapo ili kumtaka mwekezaji akabidhi hati hiyo serikalini ili ofisi yake ikaibadilishe na kwamba kama atakataa atamwandikia Rais Jakaya Kikwete kumtaka aifute hati yote.

Arsenal yapata pigo kuumia Walcott

Walcott akiondolewa nje ya uwanja baada ya kupata jeraha



Arsenal imepata pigo baada ya mchezaji wake Theo Walcott kuthibitishwa kuwa atakosa kushiriki michuano ya Kombe la dunia kwa kuwa atakuwa kando kwa takriban miezi sita baada ya kupata jeraha la mguu.

mshambuliaji huyu wa Uingereza mwenye umri wa miaka 24 alipata jeraha wakati wa michuano ya Kombe la FA siku ya jumamosi walipokutana na Tottenham na kuichapa mabao 2-0.


Taarifa ya klabu ya Arsenal imesema Walcott atafanyiwa upasuaji siku zijazo na atakua nje ya dimba kwa takriban miezi sita ambapo atakosa mechi zote zilizobaki za msimu huu sambamba na Kombe la dunia.

Michuano ya Kombe la dunia inatarajiwa kuanza tarehe 12 mwezi Juni, huku Uingereza ikitarajiwa kukipiga na Italia katika mchezo wake wa kwanza siku mbili baadae.

Rekodi ya Walcott akiwa na Kikosi cha Uingereza.

-Alionekana kwa mara ya kwanza na kikosi cha Uingereza mwaka 2006 ilipocheza na Hungary.

-Alisisimua wengi baada ya kuwa katika kikosi hicho kwenye Kombe la dunia mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 17 kabla ya kuingia kwenye ligi kuu nchini Uingereza.

-Aliwahi kufunga mabao matatu dhidi ya Croatia mwezi Septemba mwaka 2008.

-Katika hatua ya kushangaza aliachwa katika kikosi kilichocheza michuano ya kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika kusini.

Walcott alichukuliwa kutoka Southampton mwaka 2006 kwa kititta cha Pauni milioni 12.5.

Waasi wadhibiti ulinzi wa Bentiu

Waasi nchini Sudan Kusini wameanza harakati za kuulinda vikali mji wa Bentiu ambao waliutwaa kutoka kwa serikali wakiwa na hofu ya majeshi ya Serikali kuupigania.

Mwandishi wa BBC nchini humo Alastair Leithead anasema kua waasi wameanza kuleta vifaru ndani ya mji huo wenye utajiri wa mafuta huku majeshi ya serikali yakiendelea kuukaribia mji huo.
Taarifa zinazohusiana
Malefu wamekimbilia hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa nje ya Bentiu


Maelfu ya watu wametafuta hifadhi katika kambi moja ya Umoja wa Matifa viungani mwa mji wa Bentiu.

Takriban watu 1,000 wameuawa tangu mapigano kuanza tarehe 15 Disemba mwaka jana.

Takriban watu 200,000 wameachwa bila makao kutokana na mapigano Sudan Kusini.

Mgogoro huu ulianza baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani Riek Machar, kwa kupanga njama ya mapinduzi dhidi ya utawala wake . Madai aliyoyakanusga vikali.

Bwana Machar anaugwa mkono na waasi wanaoaminika kuwa 10,000, na wapiganaji wengine kutoka kabila lake.

Naye Salva Kiir anatoka katika kabila la Dinka ambalo ndilo kubwa zaidi Sudan Kusini.

Lakini viongozi hao wawili wana watu wanaowaunga mkono kutoka makundi pinzani licha ya mgogoro huo kuwa na hisia za ukabila.

Huku mzozo ukiendelea kutokota Sudan kusini na katika Jamhuri ya Afrika ya kati, mataifa ya Afrika yameanzisha jitihada za kutafuta njia za kusuluhisha mizozo hiyo.

Mkutano unaoendelea nchini Chad ni jitihada ya hivi karibuni katika kujaribu kuutatua mzozo katika Jamhuri ya Afrika ya kati, huku wanadiplomasia wa Kiafrika wanaokutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa wakijaribu kuutatua ule wa Sudan kusini.

Wapiganaji katika nchi zote wanapuuza jitihada hizo, wapiganaji waliojihami hawaonekani kuwa na hamu ya kutafuta suluhu ya kisiasa na kufikia makubaliano.

Taasisi za kieneo na kimataifa zinahusika kwa kushindwa kuchukua hatua inayohitajika kwa kasi. Lakini yanaonekana kukabiliwa na kazi kubwa katika maeneo tofauti Afrika, yalioathirika na mizozo mipya na ya zamani huko Mali, Congo , Somalia, Jamhuri ya Afrika ya kati na sasa Sudan kusini.

Monday, 6 January 2014

Dunia yaomboleza kifo cha mchezaji nguli Eusebio

Mashabiki wa soka duniani wanaomboleza kifo cha mchezaji nguli alietawala soka la Ureno katika miaka 1960, Eusebio da Silva, "chui mweusi," alifariki dunia siku ya Jumapili akiwa na umri wa miaka 71

Marehemu Eusebio da Silva Ferreira.


Eusebio da Silva Ferreira, ambaye alifariki kutokana na ugonjwa wa moyo mapema Jumapili, alitawala soka la Ureno katikati mwa miaka ya 1960, na kuiletea heshima klabu yake ya Benfica na taifa lake. Kifo chake kimesababisha kumiminika kwa salamu za rambirambi, huku serikali ya Ureno ikitangaza siku tatu za maombolezi, ambapo bendera za taifa hilo mjini Lisbon zinapepea nusu mlingoti
Mashabiki wakiwema maua na vitambaa katika sanamu ya Eusebio iliyoko katika uwanja wa klabu ya Benfica mjini Lisbon, Ureno.

Amuagiwa sifa kemkem
Rais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani Sepp Blatter alisema katika mtandao wake wa twitter kuwa mchezo wa kandanda umepoteza mtu mashuhuri, lakini akaongeza kuwa nafasi ya Eusebio katika wachezaji mashuhuri haitapotea kamwe.

Naye mchezaji mashuhuri wa Uingereza Bobby Chalton, ambaye aliisaidia Manchester United kupata ushindi dhidi ya Benfica katika fainali ya kombe la Ulaya mwaka 1968, alisema ilikuwa heshima kwake kumfahamu Eusebio.

"Aliiwakilisha timu ya taifa kwa moyo usiyo na mipaka. Sote tunakumbuka siku alipoondoka uwanjani akiililia Ureno. Machozi ya Eusebio siku hiyo ni machozi yetu leo. Taifa linalia kwa kifo chake," alisema rais wa Ureno Anibal Cavaco Silva.

Kocha wa Chelsea ya Uingereza, Jose Mourinho, ambaye ni Mreno, amemtaja Eusebio kama mchezaji wa milele, wakati naye mchezaji nyota wa Real Madrid ya Uhispania na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, akisema Eusebio ni shujaa wa siku zote.

Eusebio alifunga jumla ya magoli 733 katika mechi 745, na alishindana na wachezji nguli wa wakati huo wakiwemo Pele, Alfredo Di Stefano na Charlton. Katika mahojiano mwaka 2011, akikumbuka machozi yake baada ya Ureno kushindwa na Uingereza katika nusu fainali ya kombe la dunia mwaka 1966, Eusebio alisema: "Nilikuwa mchezaji bora wa dunia, mfungaji bora duniani na barani Ulaya. Nilifanya kila kitu isipokuwa sikufanikiwa kushinda kombe la dunia."
Eusebio akifunga bao kwa kichwa wakati wa mechi ya nusu fainali ya kombe la dunia dhidi ya Uingereza mwaka 1966.

Kutoka umaskini hadi nyota wa dunia
Akianzia katika maisha ya chini kabisa katika koloni la zamani la Ureno Msumbiji, Eusebio aliibuka kuwa moja wa shambuliaji wanaohofiwa zaidi duniani, akichanganya kasi iliyofananishwa na ya chui na uwezo mkubwa wa kushambulia.

Akitokea familia ya maskini Eusebio aliezaliwa mwaka 1942 katika jiji la Maputo wakati huo likijulikana kam Lorenco Marques, alianza kupata umaarufu katika soka la Msumbiji akiwa na klabu ya Sporting Lourenco Marques, ambayo ina mahusiano na Sporting Lisbon ya Ureno.

Kutokana na ufundi wake wa kipekee, nguvu na rekodi yake ya kufunga mabao, haikuchukuwa muda mrefu kuanza kujulikana nchini Ureno, ambako alipewa majaribio Desemba 1960 na klabu ya Sporting Lisbon, lakini ilikuwa ni kilabu ya Benfica iliomsajili .

Mashambulizi mengine Mombasa;10 wajeruhiwa

Nchini Kenya watu 10 wamejeruhiwa wakati washambuliaji waliporusha guruneti ndani ya mkahawa mmoja katika mji wa pwani wa Mombasa na kuzusha hofu ya usalama katika eneo hilo tete.

Mashambulizi yamekuwa yakiongezeka mjini Mombasa.

Mkuu wa polisi mjini Diani, Jack Ekakuro, amesema washambuliaji hao waliilenga baa moja iitwayo Tandoor mjini Diani mapema leo, wakati ilipokuwa bado imefurika watu waliokuwa wakiendelea kusherehekea mwaka mpya. Hii ni sehemu ya mlolongo wa mashambulizi, ikiwa ni pamoja na lile la bomu kwenye basi moja katika mtaa wa Eastleigh mjini Nairobi mwezi uliopita, hali inayowatia wasiwasi Wakenya wengi.
Ushindi wa vinara wa ligi kuu ya England Arsenal dhidi ya wapinzani wao wa jadi wa jiji la London,Tottenham, Jumamosi kunawapambanisha na Coventry City walio daraja la kwanza katika mzunguko wa nne wa kombe la FA.

Katika mchezo huo Arsenal iliichakaza Tottenham magoli 2-0.
Arsenal, The Gunners, ambao waliondolewa na Blackburn Rovers katika mzunguko wa tano wa mashindano kama hayo mwaka 2013, itapenda kufanya vyema ili kutwaa kombe la FA ambalo kwa mara ya mwisho ililitwaa mwaka 2005.
Taarifa zinazohusiana


Nayo Swansea, kwa kuichapa Manchester United 2-1 katika uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford, Jumapili ni fursa ya kupambana na moja wapo ya timu za Birmingham City, Bristol Rovers ya daraja la pili au Crawley ya

daraja la kwanza- huku mechi ya Crawley ya mzunguko wa pili iliyoahirishwa ikiwa bado kuchezwa.

Mabingwa watetezi wa kombe hilo Wigan wataikaribisha Crystal Palace iwapo wataifunga MK Dons katika mechi yao ya marudiano baada ya timu hizo kwenda sare ya 3-3 Jumamosi.
Ratiba ya Kombe la FA mzunguko wa nne:

Sunderland kupambana na Kidderminster au Peterborough

Bolton kupambana na Cardiff

Southampton itapambana na Yeovil

Huddersfield itakabiliana na Charlton au Oxford

Port Vale au Plymouth itachuana na Brighton

Nottingham Forest itamenyana na Ipswich au Preston

Southend na Hull

Rochdale dhidi ya Macclesfield au Sheffield Wednesday

Arsenal uso kwa uso na Coventry

Stevenage itaonyeshana kazi na Everton

Wigan au MK Dons itanyukana na Crystal Palace

Chelsea dhidi ya Stoke

Blackburn au Manchester City itapepetana na Bristol City au Watford

Bournemouth au Burton kivumbi dhidi ya Liverpool

Birmingham, Bristol Rovers au Crawley itacheza dhidi ya Swansea

Sheffield United itapambana na Norwich au Fulham

Mechi hizo za mzunguko wa nne zitachezwa kati ya tarehe 25 na 26 mwezi Januari, 2014.

Bashir kukutana na Salva Kiir

Rais wa Sudan Omar al-Bashir anatarajiwa kuwasili mjini Juba kwa mazungumzo na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuhusu mapigano yanayotokota nchini humo.

Vita vimekuwa vikiendelea nchini humo kwa zaidi ya wiki tatu huku pande zinazozozana zikikutana nchini Ethiopia kujaribu kukubaliana juu ya kusitisha vita.
Habari zinazohusiana

Hadi sasa pande hizo hazijakubaliana chochote.

Mgogoro huo ni kati ya jeshi la serikali ya Rais Kiir na waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wake Riek Machar.

Takriban watu 1,000 wameuawa tangu mapigano kuanza tarehe 15 Disemba

Vita vilianza baada ya Rais wa Sudan Kusini kumtuhumu bwana Machar kwa jaribio la mapinduzi, madai aliyoyakanusha.

Takriban watu 200,000 wameachwa bila makao,kutokana na vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vinavyosemekana kutokana na ukabila.

Aidha Bwana Kiir anatoka kabila la Dinka naye hasimu wake bwana Machar akitoka katika kabila la Nuer.

Vyombo vya habari Sudan Kusini viliripoti kuwa Rais Bashir atakwenda Juba Jumatatu kujadiliana na Rais Kiir kuhusu mzozo huo ingawa hakuna taarifa zaidi zilizotolewa.

Awali msemaji wa wizara ya mambo ya nje mjini Khartoum alisisitiza kuwa Sudan ingependa kuona kipindi salama cha kutafuta mwafaka wa amani Sudan Kusini.

Hadi Ijumaa wiki mwishoni mwa wiki, mazungumzo ya amani mjini Addis Ababa,Ethiopia, yamekuwa yakiendeshwa na wapatanishi. Lakini sasa pande zinazozozana zinatarajiwa kuanza mazungumzo ya ana kwa ana.