Thursday, 9 January 2014

PROFESA ANNA TIBAIJUKA AZOMEWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kapunga Rice Project Limited, Justin Vermaak akizungumza na Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Prof Anna Tibaijuka, alipotembelea shamba hilililopo Wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya juzi


Mbeya.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alipata wakati mgumu juzi jioni baada ya kuzomewa na wananchi waliokerwa na kitendo chake cha kubadilika na kumruhusu mwekezaji kuendelea kumiliki eneo la ardhi katika Shamba la Kapunga, Wilaya ya Mbarali, Mbeya.

Ilibidi Mkuu wa Wilaya hiyo, Gulam Hussein Kifu aingilie kati kuwatuliza wananchi hao waliokuwa wakipiga kelele na kutoa maneno makali kwa waziri huyo.

Profesa Tibaijuka alikwenda huko kwa nia ya kusuluhisha mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji wa Kampuni ya Kapunga Rice Project. Awali, shamba hilo lilikuwa mali ya Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco).

Wananchi hao walikasirishwa na hatua yake ya kuamua kuwa eneo hilo ni halali kwa mwekezaji huyo tofauti na msimamo wake wa awali wa kutaka ardhi hiyo irudishwe kwa wananchi.

Profesa Tibaijuka alibadili mawazo yake baada ya kufanya mazungumzo na mwekezaji huyo ndani ya gari akiwa na Mkuu wa Wilaya.



Msimamo awali

Profesa Tibaijuka alifika Kijiji cha Kapunga saa 6.45 mchana na kuanza kikao cha ndani na viongozi wa kijiji kwenye ofisi yao hadi saa 8.14 mchana. Alielezwa alielezwa kwamba mgogoro huo unatokana na kitendo vya mwekezaji huyo kutaka kupora ardhi yote ya kijiji chenye wakazi wapatao 4,400.

Mwenyekiti wa Kijiji, John Nyoni alisema mwaka 1995, wanakijiji walitoa hekta 5,500 za ardhi kwa Nafco ambazo ziko kwenye mradi maalumu wa kuendelea kilimo cha mpunga, lakini wanachoshangaa ni kuona aliyerithi eneo hilo (mwekezaji) anadai hekta nyingine 1,870 kutoka kwenye mashamba ya wananchi pamoja na kijiji chote.

Nyoni alidai kuwa katika harakati hizo, mwekezaji huyo alipokonya shule, zahanati ya kijiji na sasa anataka kuwaondoa wananchi wote. Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Tibaijuka alisema alifika hapo kutoa jawabu la suluhisho na kwamba atakachotoa ni cha mwisho wala hakutakuwa na mgogoro mwingine tena.

“Serikali imetambua chanzo cha makosa ni Nafco kusajili na kupata hati moja kwa eneo lote likiwamo la kijiji pamoja, hivyo mwekezaji huyo alikabidhiwa hati hiyo ikionyesha eneo la hekta 7,370 badala ya hekta 5,500,’’ alisema Profesa Tibaijuka.

Aliwahakikishia viongozi wa kijiji hicho chenye vitongoji saba kwamba alifika hapo ili kumtaka mwekezaji akabidhi hati hiyo serikalini ili ofisi yake ikaibadilishe na kwamba kama atakataa atamwandikia Rais Jakaya Kikwete kumtaka aifute hati yote.

No comments: