Mlipuko umetokea wakati wa kuadhimisha siku ya kuondolewa mamlakani kwa Hosni Mubarak
Milipuko mitatu imetikisa mji mkuu wa Misri, Cairo na kuwaua watu 5 huku zaidi ya tisini wakijeruhiwa.
Mlipuko mkubwa wa kwanza ulitokana na bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari, lililokuwa limeegeshwa nje ya kituo cha polisi.
Kundi lenye uhusiano na Al-Qaeda, Ansar Beit al-Maqdis, limekiri kutekeleza mashambulizi hayo.
Milipuko mingine miwili ilitokea nje ya kituo kimoja cha magari na kusababisha majeruhi.
Duru zinasema kuwa watu wawili waliojihami kwa bunduki waliwashambulia walinzi katika jengo hilo la polisi.
Kituo cha televisheni cha Serikali kimesema kuwa milio ya risasi ilisikika mara tu baada ya milipuko hiyo.
Moshi ulionekana ukifuka juu ya majengo katikati mwa mji na picha za televisheni zilionyesha uharibifu mkubwa wa majengo hayo.
Zaidi ya ambulansi 30 zimepelekwa eneo hilo kushughulikia waathiriwa. Mlipuko huo umetokea katika siku ya kuadhimisha miaka mitatu tangu kupinduliwa kwa Hosni Mubarak.
No comments:
Post a Comment