Thursday 23 January 2014

Mwinjilisti amuua mke wake naye ajiua kwa wivu wa mapenzi

MWINJILISTI wa Kanisa Anglikana, Eliakia Daniel (35) amekufa kwa kujinyonga baada ya kumuua mkewe, Mboni Patrick (28) kutokana na wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ulrich Matei, alisema kuwa marehemu hao walikuwa ni wakulima wa Kijiji cha Gama Makaani wilayani Bagamoyo.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu saa 10 jioni kijijini hapo ambako walikuwa wakifanya shughuli ya kuchoma mkaa.
“Mwinjilisti huyo alimuua mkewe baada ya kutokea wivu wa kimapenzi ndipo alipochukua panga na kumkata kichwani upande wa kulia na kumsababishia majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake,” alisema Kamanda Matei.
“Baada ya kumuua mkewe alimfunika kwa magogo sehemu waliokuwa wakifanyia shughuli zao hizo za kuchoma mkaa kwa ajili ya biashara. “Baada ya kumuua mkewe alijinyonga umbali wa mita 300 kutoka eneo la tukio,” alisema Kamanda Matei.
Alibainisha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni kutokana na wivu wa kimapenzi na kupelekea tukio hilo kutokea ambalo limewasikitisha wananchi wa kijiji hicho.

No comments: