MWANASIASA wa Chama cha upinzani nchini Zambia cha Alliance for a Better Zambia (ABZ), Frank Bwalya, amekamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka kwa madai ya kumkashifu rais wa nchi hiyo, Michael Satta, kwa kumwita kiazi.
Bwalya anadaiwa kumwita Rais Satta kuwa ni ‘Chumbu Mushololwa’, akimaanisha kiazi, kupitia kituo kimoja cha redio nchini humo.
Katika lugha ya Kibemba, maneno hayo yana maanisha kiazi kitamu, ambacho humegeka kinapopondwa, akimaanisha kuwa rais huyo hasikilizi ushauri wa wengine.
Aidha, taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa iwapo itathibitika kiongozi huyo wa ABZ kutoa matamshi hayo, atatiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.
Bwalya anakuwa mwanasiasa wa pili kuingia matatani baada ya mwanasiasa mwingine wa upinzani, Nevers Sekwila Mumba, wa Chama cha Movement for Multiparty Democracy kuhojiwa na polisi mwaka jana kwa kumwita Rais Satta muongo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Stephen Kampyongo, alisema Bwalya alikamatwa kwa kutoa matamshi ya kumharibia sifa Rais Satta.
Kutokana na kukamatwa kwa kiongozi huyo, kambi ya upinzani imetaka Bwalya aachiwe huru huku ikisisitiza kuwa kiongozi huyo ni mwanasiasa asiyemuogopa mtu yeyote.
Aidha, wanasiasa wa upinzani wamesema kuwa matamshi ya Bwalya si matusi kama inavyotafsiriwa. Hali ya kisiasa si shwari kwa sasa nchini Zambia kutokana na mvutano kati ya upinzani na utawala.
No comments:
Post a Comment