MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amedai kutilia shaka uwezo alionao Waziri wa Fedha, Bi. Saada Mkuya, katika kuiongoza Wizara hiyo na kudai sifa zake kitaaluma, zimegubikwa na utata mkubwa.
Prof. Lipumba aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kwa mujibu wa tovuti ya Bunge, haioneshi vyuo vya kitaaluma alivyosoma Bi. Mkuya hali inayotia shaka uwezo wake wa kuongoza Wizara nyeti kama hiyo.
Aliongeza kuwa, kama wasifu wa Bi. Mkuya uliopo katika tovuti hiyo upo sahihi ni wazi kuwa Waziri huyo hana uzoefu wa kisiasa, kitaaluma, kiutawala hata kuongoza Wizara hiyo.
"Sina hakika kama ana uelewa wakutosha kuhusu Menejimenti ya fedha za umma, upembuzi yakinifu wa miradi ya umma, athari za nakisi ya bajeti katika mfumuko wa bei, deni la Taifa, sera ya kukuza na kubadilisha mfumo wa uchumi.
"Pia sina hakika kama ana uzoefu wa kuendeleza viwanda vya ndani, kuongeza uuzaji bidhaa zetu nje ya nchi ili kuongeza ajira na ushindani katika soko la dunia," alisema Prof. Lipumba
Alisema Waziri wa Fedha anapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua sera za uchumi, kujenga hoja wakati wa majadiliano na mashirika ya kimataifa, kwenye mijadala na Mawaziri wenzake pamoja na asasi nyeti.
Prof. Lipumba alisema Serikali inakabiliwa na tatizo kubwa la fedha ambapo matumizi yanaongezeka kuliko mapato hivyo kupunguza uwezo wa Serikali kuchangia Bajeti ya Maendeleo.
Alisema nakisi (makisio) ya bajeti yameongezeka kutoka sh. bilioni 389 mwaka 2007/08 sawa na asilimia 1.7 ya pato la Taifa na kufikia sh. bilioni 2,992 mwaka 2012/13, sawa na asilimia 6.2.
Aliongeza kuwa, nchi ikiendelea na kasi ya kukopa Rais Jakaya Kikwete akiondoka madarakani, Taifa litakuwa na deni kubwa hadi kutoka nje.
"Katika sekta ya ujenzi wa barabara, makandarasi walio wengi hawajalipwa kwa wakati hivyo miradi mingi imekuwa ikisuasua, wakati mwingine Wizara husika inasaini miradi mipya wakati hakuna fedha zilizotengwa katika bajeti, Waziri wa Fedha ana wajibu wa kuweka nidhamu katika matumizi ya Serikali," alisema Prof. Lipumba.
Alisema, wakati Rais Kikwete anaingia madarakani mwaka 2005, alisema hakuna chuo kinachofundisha Uwaziri hivyo mtu yeyote anaweza kuwa Waziri ambapo mtazamo huo unachangia kuteua Mawaziri wasio na sifa za kutekeleza majukumu yao.
No comments:
Post a Comment