Thursday, 23 January 2014

Membe apigia chapua uraia wa nchi mbili Katiba mpya

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amewaomba wabunge, wasomi na Watanzania wawasaidie Bunge la Katiba ili liweze kupitisha hoja ya Watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili ili uchumi wa nchi uweze kukua.

Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam jana kwenye ufunguzi wa semina ya majadiliano ya Watanzania wanaoishi nchi za nje (Diaspora) na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

“Kuna wasomi wengi wenye utalaamu wapo nchi za nje wanafanya kazi ila wanashindwa kusaidia nchi zao kwa kuwa hawana uraia wa nchi zao,” alisema Membe.

Alisema kumruhusu Mtanzania kuwa na uraia wa nchi mbili siyo kuhatarisha usalama wa nchi. “Anayeweza kuhatarisha usalama wa nchi ni sisi viongozi. Sisi hatutetei hii hoja ya kuwa na uraia wa nchi mbili ila lazima ufike wakati tuamue kufanya hivi sio uhaini” alisema.

Alisema nchi nyingine ambazo raia wao wana uraia wa nchi mbili wamekuwa wakichangia uchumi wa nchi hizo kwa asilimia kubwa tofauti na nchi yetu.

Alitoa mfano wa nchi ya Ghana kuwa raia wake wenye uraia wa nchi mbili wamekuwa wakichangia uchumi wa nchi hiyo kila mwaka.
“Ghana wanachangia bilioni 2.1, Nigeria milioni 3.1, Kenya bilioni 1.6 ambazo ni dola za Marekani” alisema.

Alisema kwa Tanzania fedha zinazochangiwa na raia wake waliopo nje hazifiki hata 100,000 za Marekani, hali inayozorotesha uchumi wa nchi.
Upande wake, Msaidizi wa Waziri Mkuu Kitengo cha Uchumi na Uwekezaji, Suzani Mzee alisema Tanzania inaelekea kwenye uraia wa nchi mbili ambao utasaidia kuchangia maendeleo ya nchi.

“Mtanzania anayeishi nchi za nje anatoa misaada kwa kificho kwa kuwa hana uraia wa nchi yake ana uraia wa nchi anayoishi ifike wakati serikali ituunge mkono ili tuweze kuisaidia nchi yetu pasipo kificho,”alisema
Post a Comment