Monday 27 January 2014

Majambazi wampiga risasi mfanyabiashara nyumbani

Mbeya. Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamemvamia na kumjeruhi kwa risasi, mfanyabiashara maarufu wa simu jijini Mbeya, Obadia Mtawa (41).

Vitendo hivyo vimefuatiwa na kumpora mamilioni ya fedha, simu na gari la kutembelea.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni, muda mfupi baada ya Mtawa kurejea nyumbani kwake katika Mtaa wa Isyesye, akitokea katika shughuli zake katika eneo la Ilomba.

Alikuwa na gari lake lililokuwa na kasha lenye fedha na simu za aina mbalimbali.

Akizungumzia mkasa huo akiwa katika wodi ya Mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Mtawa alisema akiwa njiani kurejea nyumbani aliona pikipiki mbili zilizokuwa nyuma yake, zikiwa zimewashwa taa.

Alisema pikipiki hizo zilikuwa na watu waliokuwa wamepakizana.

Alisema baada ya kushuka kwenye gari lake akijiandaa kuingia ndani, alisikia sauti za watu wapatao wanne wakimwambia kuwa yuko chini ya ulinzi na kwamba mmoja wao aliipiga panga lake kwenye gari lake.

“Niliposhuka kwenye gari wakaingia ndani na kusema nipo chini ya ulinzi na baadaye wakapiga risasi ambazo moja ilinipiga mguuni kisha wakaniuliza fedha ziko wapi,” alinena.

Alisema aliwajibu kuwa fedha zilikuwa kwenye gari na kuwataka wazichukue. “Wakachukua funguo za gari na kisha wakaingia kwenye gari na kuoondoka nalo likiwa na fedha na simu,” alisema.

Alisema kiasi cha fedha kilichochukuliwa hakijui lakini zilikuwa za mauzo ya siku nzima ya juzi na kwamba kwa wastani maduka yake yanakusanya Sh50 milioni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba polisi walikuwa wakiwasaka watu hao.

Msangi alisema juhudi za wananchi na polisi zilifanikiwa kuliona gari la Mtawa katika maeneo ya Uyole na kwamba hadi jana hakuna mtu aliyekamatwa.
Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kuna watu waliokuwa wakimfuatilia Mtawa kwa muda mrefu.

No comments: