Tuesday 21 January 2014

Wahofu tija kwa wateule wapya


Rais Jakaya Kikwete akimuapisha Jenister Mhagama kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman

Wakitoa maoni yao jana, wadau hao walisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na kufuata sheria ili kuepuka migogoro ambayo imekuwa changamoto kubwa katika sekta hizo.

Dar es Salaam. Baadhi ya wadau wa sekta za kilimo, mifugo na mazingira wameeleza wasiwasi wao iwapo mawaziri wapya katika sekta hizo wataweza kumudu changamoto zilizopo.

Wakitoa maoni yao jana, wadau hao walisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na kufuata sheria ili kuepuka migogoro ambayo imekuwa changamoto kubwa katika sekta hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Wafugaji Nchini (Pingos Forum), Emmanuel Saringe alisema tatizo lililopo ni kutofuatwa kwa sheria za ardhi kiasi cha kuwanyima wafugaji maeneo ya malisho.

“Hatuna shida na uteuzi huo, isipokuwa tuna matarajio kwamba, sheria zitafuatwa ili kuwanufaisha wafugaji. Kwa mfano tunahitaji maeneo ya malisho yawepo kisheria na yalindwe,”alisema Saringe alipokuwa akizungumzia uteuzi wa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk Titus Kamani.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Masuala ya Ardhi, Yefred Myenzi ameungana na Saringe akisema kuwa kuna tatizo la kufuata sheria.

“Tatizo siyo uteuzi wa mawaziri bali utekelezaji wa sheria na maoni ya wadau wa ardhi. Tumeshauri sana kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, tumeshauri kuhusu mipango ya matumizi bora ya ardhi na masuala ya uwekezaji katika ardhi lakini Serikali haitekelezi,” alisema Myenzi.

Myenzi pia alisisitiza ushirikiano kati ya wizara za Kilimo, Chakula na Ushirika, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ardhi katika kupanga matumizi bora ya ardhi. Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (Jet), Deo Mfugale alisema kuwa tatizo lililopo ni mawaziri kushindwa kufuatilia utekelezaji wa sheria za ardhi na mazingira.

“Tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji ni kutofuatwa kwa sheria. Watu wanaingia msituni wanakata miti, hawachukuliwi hatua. Ukienda Bonde la Mto Kilombero, wafugaji wanafugia mtoni na wakulima wanalima bondeni lakini hawachukuliwi hatua,” alisema Mfugale.

No comments: