Friday, 31 January 2014

AU kujadili Sudan Kusini na CAR mjini Addis Ababa,Ethiopia

waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn (L) na mwenyekiti wa AU Nkosazana Dlamini-Zuma mjini Addis Ababa

Wanachama 54 wa Umoja wa Afrika wanaanza kikao muhimu nchini Ethiopia alhamisi huku wakuu wa nchi wakikabiliwa na shinikizo la kusaidia kumaliza mapigano na ongezeko la mizozo ya kibinadamu katika nchi za Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya kati-CAR.

Kabla ya ufunguzi rasmi baraza la amani na usalama la AU jumatano usiku lilikutana mjini Addis Ababa kupokea ripoti kutoka nchi zote pamoja na ripoti tofauti kuhusu mzozo wa kisiasa wa nchini Misri. Bado haiko bayana hata hivyo nchi wanachama wanaweza kufanya nini kusuluhisha mizozo.

Wiki iliyopita, pande zinazopigana huko Sudan Kusini zilitia saini sitisho tete la mapigano lakini mashahidi wanasema mapambano kati ya majeshi ya serikali na waasi yanaendelea. Maelfu ya watu wameuawa na takriban raia 800,000 wamelazimika kuondoka kwenye makazi yao tangu mapigano yazuke mwezi uliopita. wachambuzi pia wanaonya kwamba serikali ya Juba huenda ikawa haina uwezo wa kuzima ghasia.
Waasi wa kundi la Seleka huko CARWaasi wa kundi la Seleka huko CAR
AU pia itakuwa mwenyeji wa mkutano wa wafadhili siku ya jumamosi kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na operesheni za ulinzi wa amani huko Jamhuri ya Afrika ya kati-CAR.

Ghasia huko Sudan Kusini zilianza kati kati ya Disemba baada ya Rais Salva Kiir kumshutumu Makamu Rais wa zazmani Riek Machar kwa jaribio la mapinduzi dai ambalo Machar amelikanusha. Umoja wa Mataifa unasema raia 100,000 wamekimbilia nchi jirani.

Jamhuri ya Afrika ya kati imetumbukia katika ghasia mwishoni mwa mwaka jana baada ya waasi kumuangusha Rais Francois Bozize.

Zaidi ya watu 1,000 wanakhofiwa wameuawa tangu ghasia ziongezeke mjini Bangui mapema mwezi Disemba. Wafanyakazi wa misaada wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kuwa zaidi ya watu 900,000 wamelazimika kuondoka makwao.

No comments: