Wednesday 29 January 2014

Nape hajui anapambana na nani CCM

Dar es Salaam. Mwaka 2010 ulikuwa mgumu mno kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kwani alikuwa akiwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Ubungo.

Kati ya vigogo aliokuwa akipambana nao ndani ya CCM ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga na aliyekuwa mkuu wa wilaya kadhaa, Hawa Ng’umbi ambaye ndiye alishinda.

Hata hivyo, Ng’umbi alibwagwa na John Mnyika wa Chadema. Lilikuwa ni pigo kubwa mno kwa CCM na hasa kwa Nape ambaye alishajipambanua kama mpenda mageuzi ndani ya chama.

Alishajiwekea rekodi ya kufichua ufisadi ndani ya chama hicho hasa ule wa ujenzi jengo la Umoja wa Vijana pale Lumumba.

Hapo ndipo zikaanza kusikika tetesi kuwa Nape alitaka kuhamia Chadema, mara wengine wakimhusisha na chama kipya wakati huom cha CCJ (sasa CCK) kilichokuwa kikidaiwa kuanzishwa na baadhi ya vigogo wa CCM wasioridhishwa na mwenendo wa chama hicho tawala.

Lakini CCM nao walionekana kuushtukia mchezo huo. Siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 mara Nape akafutwa machozi na Rais Jakaya Kikwete alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Masasi. Ilikuwa kama gia ya kumshikilia asije kukimbilia vyama vingine.

Aliishikilia nafasi hiyo hadi mapema Machi, 2011 ambapo CCM ilifanya mabadiliko ya sekretarieti. Hapo Nape akapewa nafasi ya Katibu wa Itikadi na uenezi anayoishika hadi sasa, huku nafasi ya Katibu Mkuu akipewa Wilson Mukama.

Mabadiliko hayo yalikwenda sanjari na mkakati wa kujivua gamba. Hapo mhemko tena wa Nape na viongozi wenzake kukisafisha chama na ufisadi ukaanza pale waliposisitiza kuwa lazima wale wanaochafua sura ya chama wawajibishwe.

Sote ni mashahidi, hadi leo hakuna aliyevuliwa gamba. Chama kinaendelea kusonga mbele na magamba yake.

Juzi juzi tena baada ya sekretarieti ya chama kubadilishwa na Abdulrahman Kinana kuwa Katibu Mkuu, Nape akabebeshwa mzigo la kutaja mawaziri mizigo. Wakawashikia kidedea hadi Kamati Kuu ya CCM ili wahojiwe. Wamehojiwa lakini baadaye wamerejeshwa barazani.

Mara Nape kaibuka tena mbele ya waandishi wa habari akisema eti CCM hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha upungufu unaopigiwa kelele.

Itachukua hatua gani, wakati Mwenyekiti wa chama Rais Kikwete amesharidhika na mizigo yake? Ni kama vile Nape anatamani yeye ndiye angekuwa rais ili awafurumushe mawaziri hao, lakini basi hawezi….!
Hiyo ndiyo CCM. Utamaduni wa kuwajibishana na kufukuzana haupo. Mwenzako akifanya kosa unamezea. Kama Nape anaona kasi yake haiendani na CCM, bora atafute chama kingine ahamie.

Vinginevyo atakuwa anapiga kelele za bure huku wenzake wakiendelea kuchukua vyao mapema.

No comments: