Friday, 24 January 2014

'ICC haina ushahidi dhidi ya Kenyatta?'

Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na kesi katika mahakama ya ICC

Mahakama ya kimataifa ya ICC, imeahirisha kesi dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta anakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu anaodaiwa kuutenda wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2007.

Kenyatta amekanusha madai hayo. Baadhi ya Marais wa Afrika, wamekuwa wakilalamika kuwa mahakama hiyo inahujumu mataifa ya Afrika.

Mwendesha mkuu wa mashitaka Fatou Bensouda ndiye aliyeomba mahakama kuchelewesha kesi ya Kenyatta baada ya kupoteza mashahidi wawili wakuu.

Mmoja wa mashahidi hao alisema hataki kutoa ushahidi dhidi ya Rais Kenyatta wakati mwengine akisema kuwa alitoa ushahidi wa urongo kuhusu lililotajwa kuwa tukio muhimu sana katika kesi dhidi ya Kenyatta

Mwendesha mkuu wa mashitaka alilamizika kusitisha kesi hiyo kwa muda kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha kumpeleka Kenyatta kizimbani Hague.

Rais Uhuru Kenyatta alitarajiwa kuwa Rais wa kwanza mamlakani kufikishwa katika mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifu wa kivita

Lakini wakili wa Kenyatta ameitaka mahakama kufutilia mbali kesi hiyo.

Majaji wamezitaka pande zote, upande wa mashitaka na utetezi kufika tena mbele ya mahakama hiyo tarehe 5 Februari siku ambapo kesi ya Kenyatta ilitarajiwa kuanza kusikilizwa.

No comments: