Kikosi cha Yanga kikifanya mazoezi nchini Uturuki
BENCHI la ufundi la TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limewapa mbinu Yanga na Azam FC kama zinataka kufanikiwa katika mashindano ya Afrika.
Yanga itawakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na wataanza kucheza na klabu ya Comorozine ya Comoro na mshindi wa mechi hiyo atacheza na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri wakati Azam FC itacheza Kombe la Shirikisho kwa kuwavaa Ferroviario Da Beira ya Msumbiji.
TP Mazembe yenye wachezaji Watanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu imekuwa ikifanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika na imechukua makombe ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, 1967, 1968, 2009 na 2010 walicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Dunia na Inter Milan ya Itali ambayo ilichukua kombe.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa TP Mazembe, David Mwakasu ambaye alishangaa kuwakosa Simba kwenye michuano ya Afrika alisema: “Yanga na Azam zinaweza kufanikiwa mashindano ya Afrika kama watakuwa na maandalizi na mbinu za ushindi.”
“Jambo la kwanza ambalo kama TP Mazembe tunalizingatia ni kuwapa motisha wachezaji ambao ndiyo wafanyaji kazi wakubwa kwa kuhakikisha kila wanachohitaji wanakipata,”alisema Mwakasu.
Aliongeza: “Rais wetu, Moise Katumbi amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha timu haitetereki kwa chochote kwa kutupatia kila mahitaji, mechi za kirafiki, kambi na mahitaji yote na kama timu inapata kila kitu kwa nini ishindwe kufanya vizuri.
“Tumekuwa na maandalizi ya muda mrefu, tunaanza maandalizi mapema, kuwajua wapinzani wetu mbinu na kila kitu wanachokitumia ili tukikutana nao,tunakuwa si wageni tena, hakuna kipya kwao,”alifafanua Mwakasu.
Katika hatua nyingine, TP Mazembe ipo kwenye maandalizi ya ligi ya Congo na Ligi ya Mabingwa na tayari Samatta amesharipoti kambini, lakini Ulimwengu alitarajiwa kufika jana Jumatano kwani alitoa udhuru kuwa anauguliwa na baba yake mzazi.
TP Mazembe itaanza kucheza mechi zake za Ligi ya Mabingwa Machi na itacheza na mshindi wa mechi kati ya Astres de Douala ya Cameroon na Akounangui ya Equatorial Guinea.
Yanga ipo nchini Uturuki, ikijifua na kuafanya maandalizi ya mechi hiyo pamoja na Ligi Kuu Bara chini ya kocha mpya Mholanzi Hans Van Der Pluijm aliyerithi mikoba ya Mholanzi mwenzake, Ernest Brandts aliyetimuliwa.
No comments:
Post a Comment