Friday, 24 January 2014

Simba yajipanga upya kwaajili ya mzunguko wa pili


UONGOZI wa Simba, jana umewatangaza aliyekuwa Ofisa Habari wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga kuwa Katibu Mkuu, huku mwandishi mwandamizi Asha Muhaji kushika nafasi Ofisa Habari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage, alisema Kamati ya Utendaji ndiyo imewateua viongozi hao wapya, ili kuimarisha safu ya uongozi pamoja na kujiweka imara katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu unaotarajia kuanza kesho.
Rage alisema baada ya kuteuliwa kushika nafasi hizo, viongozi hao wanatakiwa kuanza kazi mara moja.
Mwenyekiti huyo alisema anatarajia kuitisha Mkutano Mkuu wa wanachama Machi 23, mwaka huu ambao utajadili Katiba ya klabu hiyo.
Akizungumzia barua mbili alizoandikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), juu ya marekebisho ya katiba yao na kuziba nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Rage alisema alifuata maagizo hayo na kukubaliana nayo ndipo alipoona umuhimu wa kuitisha mkutano huo.
Alisema katiba yao imeainisha kuwa wanatakiwa kufanya Mkutano Mkuu mara moja kwa mwaka, hivyo ana haki na wajibu wa kuitisha jambo hilo.
Alifafanua kuhusu kuziba nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambapo alisema Kamati ya Utendaji itazungumza na TFF kuomba wawaongezee muda, lakini kama endapo watasisitiza kufanyika kwa mkutano huo, nao hawanabudi kufanya kama walivyoagizwa.
Amewaomba wanachama wa Simba kuwa kitu kimoja, bila ya kuwagawa kama Kamati ya Utendaji walivyokubaliana ili waweze kuiboresha klabu yao.

No comments: