Thursday, 23 January 2014

wambura , Okwi stop kuichezea yanga

Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesimamisha usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda katika Klabu ya Yanga wakati likisubiri ufafanuzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Soka, Fifa.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana jana kupitia masuala mbalimbali, imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka Fifa.
Okwi ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na Fifa kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.

Hata hivyo, wakati TFF ikitoa kauli hiyo, chanzo chetu ndani ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), kimeliambia NIPASHE kuwa jina la Okwi liko katika kikosi cha wawakilishi hao wa Tanzania Bara watakaopeperusha bendera ya nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Etoile du Sahel inayoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kilieleza kuwa, hiyo ndiyo sababu iliyofanya CAF kushindwa kumuidhinisha Okwi kuichezea Yanga kutokana na jina lake kuonekana pia katika orodha ya wachezaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia.

Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa CAF inatambua Okwi ni mchezaji halali wa Etoile du Sahel na bado inasubiri maamuzi ya malalamiko ya mchezaji huyo na Klabu ya Simba yaliyopelekwa Fifa.

"Kwa mujibu wa habari ambazo nimezipata kutoka CAF zinasema kwamba walimuweka kiporo mchezaji huyo kwa sababu bado kesi yake iliyoko Fifa haijaamuliwa na pia Etoile du Sahel nayo walimuorodhesha," kilieleza.

Fifa kuna kesi nne kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi ameishitaki klabu hiyo Fifa kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.

Aidha, siku moja baada ya usajli wa Okwi Yanga, Shirikisho la Soka Uganda (Fufa) lilihitaji kujiridhisha kwa kuiandikia barua Fifa kusaka uhalali wa uhamisho wa mshambliaji huyo hatari kwenda Jangwani.

"Hivyo, TFF imeiandikia Fifa kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake," alisema Wambura.

Desemba 15, mwaka jana Yanga ilikamilisha usajili wa miaka miwili na nusu wa mshambuliaji huyo wa zamani wa watani wao wa jadi, Simba kwa dau kubwa linalotajwa kuwa Dola za Marekani 150,000 (Sh. milioni 240 za Tanzania).

Okwi, ambaye aliuzwa kwa mali kauli ya Dola za Marekani 300,00 (Sh. milioni 480) na uongozi wa Simba kwa Klabu ya Etoile du Sahel mwaka jana, ameichezea SC Villa katika Ligi Kuu ya Uganda kwa kipindi cha takriban miezi miwili na kuifungia mabao matatu. Pia ameichezea Yanga katika mechi tano za kirafiki tangu ajiunge nayo akiifungia mabao matatu.

Ikumbukwe kuwa Novemba mwaka jana Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliwataarifa Fufa kutowatumia Okwi na beki Godfrey Walusimbi (24), katika mashindano ya CHAN yanayoendelea nchini Afrika Kusini kwa sababu wawili hao hawana uhalali wa kukipiga katika mashindano hayo yanayoshirikisha wachezaji wa ndani kwa kuwa bado wana kesi ambazo hazijamalizika na timu zao za Etoile du Sahel na Don Bosco ya DR Congo.

Lakini, Mkurugenzi wa SC Villa, Edgar Agaba, aliuambia mtandao wa MNTfootball Desemba 17 mwaka jana kuwa Okwi (20), amejiunga na vinara wa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga akiwa mchezaji huru.

YANGA WANENA
Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema bado hawajapata taarifa rasmi kuhusu suala hilo.
"Mimi ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako, hatuna taarifa rasmi za kuzuiwa kwa usajili wa mchezaji wetu (Okwi).

Tukipata tutatoa tamko," alisema Njovu. Hata hivyo, mara tu baada ya kufanikisha kumsajili Okwi, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, alisema hawakukurupuka katika kumsajili mkali huyo wa kufumania nyavu za timu pinzani.

Bin Kleb alisema walimsajili Okwi siku sita kabla ya kupata Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) Desemba 15, mwaka jana, ndipo wakaamua kutangaza rasmi usajili huo.

Kuhusu utata wa sakata la straika huyo na Etoile ambalo limefika hadi Fifa, Bin Kleb alisema: “Tumefuatilia kote, hadi kwa wanasheria na tumefanikiwa kupata ITC yake, nawaambia mashabiki wa Yanga wajue viongozi wao wanafanya kazi. Hatuna stori nyingi, sisi tunafanya vitendo na kazi zetu kwa umakini."

“Tumepitia sehemu zote, tumeona kabisa tuko sahihi katika kumsajili mchezaji huyo na hakutakuwa na tatizo lolote upande wetu,”alifafanua zaidi kiongozi huyo aliyefanikisha pia usajili wa nyota kadhaa wa Yanga akiwamo 'kiraka' Mbuyu Twite.
Post a Comment