Sunday 26 January 2014

Logarusic amtimua Owino kambini

SIMBA imeingia kambini na wachezaji 19 bila ya beki wake wa Uganda, Joseph Owino ambaye alikosana na kocha Zdravko Logarusik mazoezini juzi Alhamisi.

Timu hiyo imeingia kambini katika Hoteli ya Vinna, Mburahati, Dar es Salaam.

Tukio hilo limetokea wakati Simba kesho Jumapili ikiwa tayari kwa mzunguko wa pili ikiikabili Rhino Rangers ya Tabora, lakini cha kushtua ni kwamba beki wa Msimbazi, Joseph Owino ametibuana na bosi wake, Logarusic.

Owino alitibuana na Logarusic katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam na kumtoa kabisa nje ya uwanja na kuacha wengine wakiendelea jambo ambalo huenda likamtoa mchezaji huyo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kwa muda.

Kwa mujibu wachezaji waliokuwa karibu na Owino mazoezini wanadai kuwa kocha huyo alimtolea Owino lugha mbaya iliyomkera mchezaji huyo na kumuondoa mchezoni ndio maana akamsihi bosi huyo asimuelekeze kwa kumtukana bali amueleweshe kwa lugha ya kiungwana ndipo picha lilipoanzia.

Wachezaji wenzie wanadai baada ya Owino kutukanwa hilo alitoka nje ya uwanja na kuvua vifaa vya mazoezi, lakini kocha mwenyewe anadai kwamba yeye ndiye aliyemtoa mchezaji huyo mazoezini. “Hii si mara ya kwanza kwa Owino kulalamika kuhusiana na kocha huyo kumtukana mazoezini anapokwenda kinyume na maelekezo yake, lakini aliendelea. Safari hii ameshindwa kuvumilia na kufokeana naye kisha akavua bipsi na kutoka nje,”alidai mmoja wa wachezaji wa Simba.

Alipoulizwa kocha huyo alisema alimtoa Owino kwavile alikuwa hafuati maelekezo yake wala hakumtukana.

Logarusic alisema mara nyingi beki huyo anacheza bila kufuata maelekezo yake kama ilivyojitokeza katika mazoezi hayo. “Owino nimemtoa uwanjani katika mazoezi yangu kutokana na kucheza bila ya kufuata maelekezo yangu, kama beki anatakiwa kutambua wajibu wake na kufuata maelekezo.

“Siwezi nikawa na beki asiye na nidhamu ya ukabaji, anatakiwa afuate maagizo yangu jinsi ya kukaba na kupambana na timu pinzani, nimemwambia afanye mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi atakuwa na msaidizi wangu Matola (Selemani) na jioni nitakuwa naye pia ili abadilike,”alisisitiza kocha huyo asiye na masihara kwenye nidhamu ya wachezaji na uwajibikaji uwanjani.

Kuhusu kikosi kitakachocheza kesho alisema: “Sijaamua lakini ninao wachezaji 18 wote wapo fiti.”

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ alisema kuwa “Hatuwezi kulitolea tamko suala hilo mpaka tupate ripoti kamili ya kocha.”Logarusic amtimua Owino kambini

No comments: