Beki wa Zimbabwe 'Warriors', Kudakwashe Mahachi, aliwapa wakati mgumu Mali baada ya kuwatoka mabeki wao wanne na kufunga bao safi la pili lililoifanya nchi kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani 'CHAN' katika mechi ya robo fainali iliyochezwa juzi.
Mbele ya macho ya washabiki wengi wa Zimbabwe, beki huyo aliyebarikiwa kutumia mguu wa kushoto alikimbia na mpira akiwatoka mabeki hao kuelekea golini kwa Mali katika dakika ya saba ya kipindi cha pili kabla ya kuachia shuti lililompita kipa Diakite ambaye alishindwa la kufanya kuisaidia nchi yake ya Mali isifungwe bao hilo.
Zimbabwe imetinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 2-1 huku katika mechi zake tatu zilizotangulia katika michuano hiyo ikiwa haijaruhusu bao hata moja kwenye goli lake.
Mchezaji Ibourahima Sidibe wa Mali alipata nafasi nzuri ya kufunga bao ndani ya dakika tatu za mwanzo za mechi hiyo, lakini George Chigova alienda chini kifundi kuzuia mpira usitinge kwenye nyavu za nchi yake.
Zimbabwe ilipata bao lake la kwanza katika dakika ya 11 wakati Simba Sithole alipompita Souleymane Konate kabla ya kupiga shuti la chini lililompita kipa Soumaila Diakite.
Katika dakika ya 24, Diakite alifanya kazi nzuri kuzuia shuti la mpira uliosafiri umbali mrefu usiingie golini kwake ambapo kidogo ungeipatia Zimbabwe bao la pili kupitia kwa Peter Moyo.
Zimbabwe iliendelea kuongeza mashambulizi kwa wapinzani wao, lakini hawakuweza kuongeza bao la pili katika dakika 45 za kwanza kutokana na jitihada kubwa za kipa wa Mali, Diakite.
Lassan Diara alipoteza nafasi murua ya kusawazisha katika muda uliokaribia mapumziko wakati shuti lake kali lilipopiga juu ya mwamba wa goli.
Lakini vijana wa Ian Gorowa waliamka na kuanza kushambulia zaidi kipindi cha pili walipopata bao la pili kupitia kwa beki Mahachi.
Viungo wa Zimbabwe walifanikiwa kumiliki sana mipira katika mechi hiyo, lakini Mali hawakukatishwa tamaa ya kuendelea kutafuta mabao.
Hata hivyo, Mali walipoteza nafasi nzuri zaidi katika dakika ya 75 baada ya Hamidou Sinayoko alipojaribu kupiga mpira ulioenda pembeni akiwa na nia ya dhati kabisa ya kummaliza kipa Chigova wa Zimbabwe.
Diakite aliendelea kuiokoa nchi yake isioge mabao baada ya kuokoa mchomo dakika ya 84 wakati alipopangua mpira wa Masimba Mambare na kusababisha kona ambyo haikuzaa bao.
Mali wangeweza kusawazisha tena dakika ya 88, lakini mpira wa chini uliopigwa na Sinayoko ulizuiwa kifundi na Chigova na kuwa kona ambayo Sinayoko aliipatia bao la kufutia machozi Mali.
Kwa ushindi huo, Zimbabwe imefuzu nusu fainali katika michuano hiyo inayofanyika Afrika Kusini pamoja na Nigeria ambapo, washindi wengine wawili wa kuungana nao hatua ya nusu fainali walitarajiwa kujulikana jana, usiku baada ya mechi kati ya Gabon na Libya na nyingine kati ya Ghana dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrais ya Congo (DRC).
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, ameipongeza 'Super Eagles' kwa ushindi wa kishujaa ambapo, walifanikiwa kuzawazisha mabao matatu na kushinda kwa mabao 4-3 dhidi Morocco katika mechi nyingine ya robo fainali iliyochezwa juzi mjini Cape Town.
Hadi mapumziko, Morocco walikuwa wakiongoza kwa mabao 3-0 katika mechi hiyo.
Rais Jonathan kupitia maelezo yake yaliyosainiwa na Reuben Abati ambaye ni Mshauri Maalumu wa Rais (habari na uchapishaji), alipongeza ushindani uliooneshwa na wachezaji wa nchi yake ambapo, Super Eagles walishindana na kufanikiwa kuzawazisha mabao 3 hadi kuongeza bao la nne na kufanikiwa kutinga nusu fainali.
Katika pongezi hizo, Rais Jonathan aliwamwagia sifa Super Eagles kwa moyo wao wa kujituma, uzalendo na kujitolea kwa taifa lao.
Alisisitiza kwamba, wachezaji hao waendelee na moyo huo kwa ajili ya taifa lao mpaka ushindi wa mwisho upatikane katika michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani barani Afrika.
Pia, Rais Jonathan aliwahakikishia Super Eagles kwamba, wataendelea kupata mchango wa kila hali kutoka kwa serikali ya shirikisho pamoja na Wanigeria wote wakati wakiendelea kupambana kuhakikisha kuwa, wanaongeza taji hilo baada ya kushinda lile Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka jana.
Rais huyo aliungana na wananchi wote wazalendo waliofurahishwa na ushindi huo kuwaombea washinde mechi inayofuatia ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Katika mechi hiyo, mabao ya Nigeria yalifungwa na U. Uzochukwu (dakika ya 49), R. Ali (dakika ya 55), E. Uzoenyi (dakika ya 90) na A. Ibrahim (dakika ya 111).
Mabao ya Morocco yalifungwa na M. Moutouali (dakika ya 33), M. Iajour (dakika ya 37) na M. Mouto
(dakika ya 40).
Hadi tunakwenda mitamboni, Gabon ilikuwa nguvu sawa na Libya kwa bao 1-1 dakika ya 75 katika mechi ya robo fainali nyingine iliyoanza saa 12 jioni, jana huku DRC ikitarajiwa kupambana na Ghana katika mechi kali nyingine ya robo fainali iliyotatarajiwa kupigwa kuanzia saa 3:30 jana pia.
Mechi za nufu faiinali zimepangwa kuchezwa Januari 29.
No comments:
Post a Comment