Monday 27 January 2014

Tuzo ya Tanzania Boxing Award' yaangukia kwa CHEKA

NGULI wa masumbwi nchini, Francis Cheka ameng'ara katika tuzo za Ngumi za 'Tanzania Boxing Award' baada ya kunyakua tuzo mbili katika hafla hiyo.
Cheka bondia pekee aliyeonekana kivutio katika tuzo hizo amenyakua tuzo ya bondia bora wa mwaka 2013 na bondia bora wa ngumi za kulipwa kwa mwaka huo.
Akizungumza mara baada ya kunyakua tuzo hizo, Cheka ameushukuru uongozi wa BFT kwa kuandaa tuzo hizo na kufanyika kwa mara ya kwanza kwa kuwa hapo awali zilikuwa zikitangazwa huku wahusika wakiingia mitini.
Cheka alisema amefarijika sana kutwaa tuzo hizo kwani inaonesha wazi wadau wanatambua mchango wake katika tasnia hiyo ya masumbwi nchini.
Alisema endapo utoaji tuzo hizo ukiendelea kufanywa utahamasisha mabondia wachanga waweze kushiriki kwa wingi katika mchezo huo kwani wataona mchango wao unathaminika tofauti na zamani.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alisema tuzo hizo zimekuja wakati mwafaka kwa kuwa yeye ni kipenzi cha wanamichezo na amefanikiwa kuwa Naibu waziri wao.
Nkamia alisema atatoa ushirikiano kwa BFT kwa kuwa wameonesha moyo wa kufufua mchezo huo kwa kasi kubwa.
Waziri huyo amesikitishwa na ulingo unaotumiwa na mabondia wa Tanzania katika kufanyia mashindano mbalimbali kwani hauna hadhi kabisa ya kutumika katika michuano hiyo.
"Tanzania ina mabondia wengi wazuri ambao wanawakilisha nchi kimataifa, ni aibu kuona ulingo wanaotumia kupata mabondia hao haukidhi vigezo vyovyote," alisema Nkamia.
Nkamia ameahidi kutatua matatizo ya wanamichezo pale inapobidi kwa kuwa hata yeye ana uchungu mkubwa anapoona wanamichezo wa Tanzania wanafanya maandalizi katika mazingira magumu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa tuzo hizo, Mutta Lwakatare ambaye pia ni Rais wa BFT, amewaahidi wanamasumbwi kuendelea kuboresha tuzo hizo mwaka hadi mwaka na kwamba mapungufu mengi yaliyojitokeza katika tuzo hizo hayatajirudia kwa kuwa huo ulikuwa ni mwanzo tu.
Lwakatare alisema uongozi wake utajipanga kuboresha masumbwi kwa kuwa wanachama hai wa shirikisho hilo kwa sasa ni wachache hivyo kuhakikisha wanafufua uhai wa wanachama wao.
"Tuna klabu nyingi sana za ngumi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara lakini klabu hai zilizosajiliwa ni chache sana hivyo ipo haja ya kuhakikisha uhai wa klabu tulizonazo unakuwepo kwa kila mkoa ili iwe rahisi kupata mabondia kutoka mikoa yote Tanzania Bara," alisema Lwakatare.

No comments: