Saturday, 18 January 2014

Wagundua sumu ya kuua VVU mwilini

Timu ya Watafiti katika Chuo Kikuu cha North Carolina nchini Marekani, wamegundua aina ya sumu ambayo ina uwezo wa kuua seli ambazo zimekwishaathiriwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Sumu hiyo iliyopewa jina, 3B3-PE38, inaweza kutumika kutengeneza dawa ambayo ikitumiwa na mtu aliyeathirika kwa VVU, itasaidia kuua virusi.

Watafiti wamebaini pia kuwa dawa hiyo itaweza kusaidia waathirika kutolazimika kutumia dawa za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARVs) maisha yao yote.

Hii ni mara ya kwanza kwa wanasayansi kuweza kugundua sumu maalumu ya kuua VVU. Tafiti nyingi zinazoendelea sehemu nyingi duniani ni za kupata chanjo.

Kwa kawaida dawa ni sumu inayoua au kuathiri kiumbe kilichokusudiwa wakati chanjo ni njia ya kuufanya mwili kutengeneza wenyewe kinga dhidi ya vimelea, kulingana na aina ya ugonjwa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa wiki hii na Taasisi ya Tafiti za Kukabili Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID) ya Marekani, inasema ni ugunduzi wa kipekee.

Upekee huo unaoelezwa unatokana na ukweli kuwa kwa sasa dawa zilizopo za ARV zina uwezo wa kuzuia seli nyeupe iliyoshambuliwa isimamishe mvumo wa kuzalisha virusi.

Walivyoendesha utafiti

Utafiti huo uliofadhiliwa na Taasisi ya Afya ya Taifa (NIH) ya Marekani, unaelezwa kuwa panya 40 walitumika katika kutafiti 3B3-PE38.

Walichofanya watafiti hao ni kuwagawa panya kwenye makundi kadhaa na kupewa dozi ya sumu ya 3B3-PE38 kwa viwango na muda tofauti kuanzia wiki mbili hadi nne.

Baadhi walipewa ARV pekee na wengine walipewa pamoja na sumu hiyo ya 3B3-PE38.

Katika utafiti huo, walibaini kwamba wale ambao walitumia ARV pamoja na sumu hiyo, waliweza kupunguza kwa kiwango kikubwa VVU pamoja na seli ambazo tayari zimeathirika.Taarifa za awali zinaelezwa kuwa sumu hiyo inaweza kusaidia kutibu watu walioathirika na mojawapo ya aina ya VVU.

No comments: