Friday 24 January 2014

Simanzi Sekondari ya Sabodo, wanafunzi wazikwa

Mtwara. Simanzi na huzuni vimetawaka katika Shule ya Sekondari ya Mustapha Sabodo baada ya kutokea vifo vya wanafunzi watano vilivyosababishwa na ajali ya gari juzi.

Wanafunzi watano wa shule hiyo, walifariki kwa ajali ya gari huku 46 wakijeruhiwa na kati ya hayo, wanafunzi 20 waliumia vibaya na kuhitaji huduma za upasuaji. Waliofariki ni Khairath Mohammed, Mwanahamisi Mohammed, Hasma Mpunja, Hilda Mathias na Farida Ally ambao wote walizikwa jana.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Shaibu Maarifa alisema jana kuwa hadi kufikia jana jioni, hakukuwa na ongezeko la vifo na kuwa majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Ligula na Hospitali ya Misheni ya Nyangao.

Alisema kuwa majeruhi waliokuwa wamebaki hospitalini hapo ni 20 na kwamba watatu wamehamishiwa katika Hospitali ya Mission ya Nyangao ili kuokoa muda wa kusubiria foleni kwa ajili ya upasuaji na wengine watano tunatarajiwa kuruhusiwa na wengine watabaki kwa uangalizi.

“ Majeruhi wetu wanaendelea vizuri, tuliendelea kuwahudumia kwa kushirikiana na wenzetu wa Hospitali ya Nyangao...,” alisema Dk Maarifa.

Dk Maarifa aliongeza kuwa kutokana na ajali hiyo zilihitajika damu salama chupa 25 na kwamba ziliweza kupatikana kwa haraka kutoka katika Kituo cha Damu Salama cha Kanda ya Kusini ambacho makao yake ni hospitalini hapo.

Rose Godwin (14) mmoja wa majeruhi aliyevunjika mkono wa kushoto, akielezea mkasa huo, anasema: “Tulikuwa kwenye mchakamchaka na wakati tunasubiri kuchukuliwa namba ili turudi shuleni wakati huo tukiwa tumejipanga mstari jirani na shule ndipo nikaona gari lililokuwa linatoka Mkoa wa Lindi na lingine Mtwara sikumbuki ilikuwaje, wakagongwa na mimi nikajikuta naanguka na kuvunjika mkono.”

Eva Issaya, alisema: “Chanzo cha ajali ni magari mawili kushindwa kupishana kutokana na barabara kuwa nyembamba na katika kupishana na sisi tukiwa pembeni ya barabara gari moja likawagonga baadhi ya wanafunzi waliokuwa njiani na sisi likatuangusha.”

Nao wakazi wa Kijiji cha Msijute jirani na ilipotokea ajali hiyo, waliiomba Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara, Tanroads kuangalia namna ya kupunguza ajali kwa kuweka matuta eneo hilo.

“Tumepoteza vijana wetu wadogo ambao ndiyo taifa tegemezi ambao ndiyo walikuwa wanaandaa maisha yao ila cha msingi tunaiomba Serikali na hawa Tanroads watuwekee matuta na tahadhari kwani eneo hili kwa sasa lina mwingiliano mkubwa wa watu na magari hasa tangu ilipoanzwa ujenzi wa kiwanda hiki cha saruji cha Dangote,” alisema Juma Namkopi.

Akizungumza Ofisa Uhamasishaji kutoka Mfuko wa Damu Salama wa Kanda ya Kusini,

Anania Lwoga alisema kuwa watu wanatakiwa kujitokeza kushiriki uchangiaji damu salama kwani huhitajika muda wote.
Akizungumza jana, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mustapha Ulaya alisema kuwa ni majonzi na simanzi shuleni kwake na kwa sasa wamesitisha masomo kuomboleza msiba huo mkubwa kuikumba shule hiyo.

“Tumesitisha kufundisha kwa muda, kila mmoja anatafakari hali ilivyokuwa katika ile ajali. Ni watoto wengi kuumia na kufa, imetushtua hali hii,” alisema Mwalimu Ulaya.

Hata hivyo alisema kuwa ana matumaini ya vijana wake kupata nafuu mapema na kurudi shuleni kuendelea na masomo.

Alisema pia kuwa hawataacha mchakamchaka kwa kuwa ni utaratibu wa shule hiyo tangu ilipoanzishwa kwani ni sehemu ya kuwatayarisha wanafunzi kwa siku.

No comments: