Kutumia alama ya Ndizi na Chungwa
*Nia ni kuhakikisha serikali mbili zinabaki
*Yamshushia lawama nzito Jaji Warioba
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kipo katika mkakati mzito wa kuhakikisha kinakwamisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya yenye muundo wa serikali tatu, imeelezwa.
Hatua hiyo inakuja baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, kuwasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, rasimu ya pili ya Katiba Mpya yenye mapendekezo ya muundo wa serikali tatu.
Kitendo cha rasimu hiyo kuendelea kuwa na mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, kimeonesha kuwakera vigogo wengi wa CCM, ambapo katika kuhakikisha suala hilo halifanikiwi tayari harakati mbalimbali zimeanzishwa ili kuhakikisha Bunge Maalumu la Katiba linakiondoa kipengele hicho na kuweka cha serikali mbili.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka CCM, zimeweka wazi kwamba baadhi ya viongozi wa chama hicho wamebaini kwamba mapendekezo ya serikali tatu yana mkono wa baadhi ya wajumbe wa tume ya mabadiliko ya Katiba pamoja na Mwenyekiti wao na kwamba wameamua kufanya hivyo kwa maslahi yao au ya watu wao.
“Baadhi ya viongozi wa chama wamefanya mazungumzo ya kina na Jaji Warioba, wamegundua ipo namna, wameona kuna wajumbe wa tume wana maslahi kwenye suala hili la muundo wa serikali tatu, nia ya CCM si kukwamisha Katiba, dhamira kubwa ni kuondoa kipengele cha serikali tatu”alisema mtoa habari wetu.
Alisema katika kuhakikisha mipango hiyo ya chama inafanikiwa, juzi viongozi wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa iliyokutana visiwani Zanzibar mbali ya kujadili suala la mgombea uwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki, pia walilijadili suala la Katiba Mpya na Muundo wa serikali tatu, ambapo upo uamuzi ambao umefikiwa na utawekwa wazi muda utakapofika.
Aidha alieleza kuwa kinachofanyika sasa ndani ya CCM ni kuhakikisha unaundwa mkakati kabambe wa kulikamata Bunge la Katiba ili kuhakikisha linang’oa kipengele cha serikali tatu.
Endapo mkakati huo utashindwa kufanya kazi, upo mkakati mwingine wa kutumia alama za ndizi (kambi ya ndiyo) na chungwa (kambi ya hapana) ili kufanikisha mpango wa kuondoa kipengele cha muundo wa serikali tatu.
Asili ya alama za chungwa na ndizi ni ya nchini Kenya, ambapo alama hizo zilitumika kupinga pendekezo la Katiba Mpya iliyopendekezwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Mwai Kibaki na wafuasi wake.
Katika kuhakikisha katiba hiyo haipiti, chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kilianzisha mchakato wa kupata maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya.
Katika mchakato huo upande uliokuwa ukitumia alama ya chungwa ulifanikiwa kuipinga Katiba hiyo hali iliyosababisha Rais Kibaki aliyekuwa upande wa ndizi kuwaondoa madarakani viongozi wote wa serikali yake waliounga mkono kambi ya chungwa.
Mfumo huo umeonekana kuivutia CCM ambayo inajiamini kwamba ina wafuasi wengi na kama wataamua kuibuka na rasimu yao na kuipeleka kwa wananchi kwa mfumo wa chungwa na ndizi ni wazi watashinda.
Imebainishwa kwamba nia ya kupinga muundo wa serikali tatu ni kuiepusha nchi na vunjiko la muungano, lakini pia kuwaondolea mzigo wananchi katika kuziendesha serikali hizo.
Msimamo wa wanaCCM wengi ni kuendelea na muundo wa serikali mbili na kwamba muundo wa serikali tatu ambao utairejesha Tanganyika unaonekana kuwa ni kaburi la Muungano.
Harakati za wanaCCM kuupinga muungano zilianza muda mrefu tangu ilipotolewa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya.
Baadhi ya wanaCCM wanaoupinga muundo wa serikali tatu ni Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu wa zamani Cleopa Msuya, Rais wa Zanzibar Dk. Shein na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Hata hivyo hali ni tofauti kwa baadhi ya makada wa chama hicho, ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye kwa upande wake anakubaliana na mfumo wa serikali tatu.
MTANZANIA Jumatano lilifanya mazungumzo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, juu ya chama chake kuhusishwa na mkakati wa kuvuruga mchakato wa Katiba Mpya, ambapo alisema hawana mpango huo ingawa msimamo wao ni serikali mbili.
“Msimamo wa chama chetu uko wazi katika hili, kila wakati tunasema CCM inaamini katika Serikali mbili na si tatu. Lakini katika hili tunahisi kuna jambo limejificha na sasa tunajipanga kwenda katika vikao kwa ajili ya kujadili kwa kina suala hili.
“CCM inahitaji kujua takwimu sahihi, inakuwaje Tume ya Jaji Warioba inaeleza waliokubali Serikali ya mkataba je, mbona haisemwi waliotaka Serikali mbili.
“Hapa kuna jambo na CCM haiwezi kukubali jambo hili. Suala la kukwamisha katiba kila mtu atasema lake, lakini tambua kuwa CCM ina wajumbe wengi katika Bunge kuliko chama chochote cha siasa,” alisema Nape.
MTANZANIA Jumatano lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano, Habari na Uenezi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Mnyika ili kutoa maoni yake juu ya mikakati ya CCM, ambapo alisema tangu mchakato wa Katiba Mpya ulipoanza chama hicho tawala kimekuwa kikiupinga muundo wa serikali tatu ambao umependekezwa na wananchi.
“Mpango wa CCM kukwamisha muundo wa Muungano wa Serikali tatu unapaswa kuanikwa hadharani kabla ya Bunge la Katiba kuanza ili wananchi waweze kukibana chama hicho, viongozi wake na wabunge wanaotokana na chama hicho wanapaswa kuheshimu maoni ya wananchi wanaotaka maboresho ya muundo na mfumo wa muungano.
“Mipango hiyo isipojadiliwa kuanzia sasa, CCM itatumia uwingi wake vibaya ndani ya Bunge la Katiba kupitia wabunge wanaotokana na chama hicho kuhodhi mchakato na kuchakachua rasimu ya katiba,”alisema.
Alieleza kuwa maamuzi katika Bunge yatafanywa kwa kura kwa kila upande wa muungano, hivyo makundi, taasisi na watu wenye malengo yanayofanana ambao wajumbe wake watateuliwa ni lazima wajiandae kudhibiti mipango haramu ya CCM kwa kuwa katiba ni ya watanzania wote na si ya chama kimoja.
No comments:
Post a Comment