Friday, 31 January 2014

Malecela amchambua Lowasa

MAKAMU Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Taifa, John Samwel Malecela, ameitaka Sekretarieti ya chama hicho kuchukua hatua za haraka dhidi ya wanachama wanaoharibu misingi ya chama hicho kwa kutumia fedha zao hadharani kwa lengo la kutafuta umaarufu na ushawishi kwa vijana katika harakati za kugombea urais mwaka 2015.
Ushauri huo ulitolewa jana mjini hapa na Malecela wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mbio za urais ndani ya chama hicho wakati muda ukiwa bado.
Malecela alisema kuwa wanachama wa chama hicho wamekuwa njia panda, huku wakitamani kujua tamko au karipio la chama juu ya suala hilo la harakati za urais mwaka 2015 bila mafanikio.
Alisema ni lazima Sekretarieti ya chama ibadilike na kuchukua hatua mara moja ili kuleta imani kwa wanachama wake.
“Ninaomba niseme bila kuwa na karipio au tamko hawa wanaotumia fedha zao hadharani kwa lengo la kutafuta umaarufu na ushawishi kwa vijana ili kupata madaraka wanaharibu misingi yetu bora ya uongozi iliyowekwa na waasisi wetu ndani ya chama,” alisema Malecela.
Aliongeza kuwa kipindi cha nyuma viongozi wa chama hicho hawakuongozwa na fedha kutafuta madaraka, bali nidhamu, busara na uchungu wa rasilimali za taifa.
"Hivyo, ndivyo vilivyowezesha kuongoza taifa ikiwa ni pamoja na kufuata misingi na maadili ya uongozi ndani ya chama na serikali," alisema na kuongeza kuwa;
"Viongozi wa zamani wamekuwa wakiumia sana kuona chama kinataka kutekwa na wenye fedha kwa uchu wa madaraka hali inayowafanya kujiuliza wanakopata fedha hizo pamoja na masilahi ya madaraka wanayotaka kununua ni ya nani, wakati Watanzania wakiendelea kuwa masikini."
Malecela alisisitiza kuwa; “Tunaumia sana kuona chama sasa kinataka kutekwa na wenye fedha kwa uchu wa madaraka hadi tunashangaa na kujiuliza hizi fedha wanazipata wapi.
Madaraka wanayotaka kwa kununua ni kwa masilahi ya nani huku Watanzania wakiendelea kuwa maskini?”
Malecela alipongeza juhudi za Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Paul Makonda, na kusema kuwa anamuunga mkono kwa kitendo chake cha kumkemea Mbunge wa Monduli,Edward Lowassa, kwa kukiuka misingi ya katiba ya chama na kuvuruga chama kwa lengo la kutaka urais mwaka 2015.
“Nadiriki kusema nampongeza na kumuunga mkono kijana huyu (Makonda) kwa kauli zake nzito na za kijasiri kwa masilahi ya CCM kwa kuweza kumkemea, Lowassa, bila kujali cheo na umaarufu wake kwa jinsi anavyokivuruga chama chetu kwa lengo la kutaka urais mwaka 2015, huku Sekretarieti ya chama ikiwa imekaa kimya wakati inajua muda wa kuanza mbio hizo bado na kufanya hivi kwa sasa ni kukiuka misingi ya katiba ya chama,” alisema Malecela.
Alibainisha kuwa anasikitishwa kuona juhudi za uongozi wa sasa wa chama ngazi ya juu ikiwa ni pamoja na Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana na Katibu wake Nape Nnauye za kutetea chama hicho zikibezwa na baadhi ya watu wenye lengo la kutaka kuharibu chama.
Wakati huo huo, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, ameishukia UVCCM kwa kuwahusisha viongozi wa dini na mbio za urais wa mwaka 2015.
Akizungumza na Waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Shekhe Salum, alisema kuwa kauli iliyotolewa na Makonda imewagusa hivyo ni lazima aijibu.
Alisema ikizingatiwa kuwa yeye ni Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, hawatujui Makonda amewahusishaje viongozi wa dini na mambo ya kampeni za urais mwaka 2015 hazijaanza na hakuna hata mtu mmoja aliyetangaza kugombea nafasi hiyo.
"Wasiwasi wa kumuogopa Lowassa unatoka wapi? Kama yeye anawajua wanaogombea urais kuwaambia Watanzania kuwa huyo hafai mbona hatuambii anayefaa ni nani?" alihoji.
Alihoji ni wapi Makonda amepata kazi ya kuwachagulia Watanzania Rais anayefaa amepewa na nani? aliendelea kusema; "Kosa la viongozi wa dini ni nini, maana kama kualikwa kwenye makanisa au misikiti kufanya harambee mbalimbali wanasiasa wote wanaotajwa kuwa wanaweza kugombea urais wanaalikwa, kwa nini viongozi wa dini walaumiwe kwa ajili ya Lowassa?."
Alisemaa namkumbusha Makonda kuwa, Lowassa amekuwa kiongozi katika awamu zote za utawala wa nchi hii, hivyo anaposema hafai ina maana yeye anamjua zaidi kuliko marais wote.
Katika hatua nyingine, Shekhe Salum alisema kuwa kushambuliwa kwa Mawaziri na kuwaita Mizigo ni ukosefu wa maadili na huko ni kumtukana aliyewateua.
Alisema wanaamini kuwa Rais hakukurupuka kufanya uteuzi huo, lakini hao wanaowakashfu mawaziri ambao pia ni wabunge kuwa mizigo wao wanao uwezo wa kumfikia yule aliyewateua na wanajua kuwa anaweza akabadilisha uteuzi huo, hivyo wangemshauri mwenyekiti wao wa taifa (Rais Jakaya Kikwete) ili awawajibishe badala ya kuwakashfu kupitia vyombo vya habari.
Juzi Makonda, alimshukia Lowassa akimtuhumu kutumia watu kukigawa chama na watu kwa ajili ya tamaa ya urais mwaka 2015. Hata hivyo, kauli hiyo ya makonda imepokewa kwa hisia tofauti na kuzidisha malumbano ya kisiasa ndani ya chama hicho.

No comments: