Wednesday 29 January 2014

Dk slaa ampa vidoge J k kuhusu safari zake za mara kwa mara

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, ameitaka Serikali kutoa kauli juu ya madai ya ufujwaji wa fedha kwenye safari za nje hasa zinazohusu msafara wa Rais Jakaya Kikwete, akisema zingeweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi wake, hususan watumishi.

Dk. Slaa amesema tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2010, amefanya safari za nje ya nchi zipatazo 358, huku kila safari ikigharimu takribani milioni 500, akisema fedha hizo zingeweza kusaidia katika kuboresha hali ya watumishi nchini.

Akizungumza katika mfululizo wa mikutano ya chama hicho iliyopewa jina la M4C- Operesheni Pamoja Daima jana katika maeneo ya Uyovu (Bukombe), Kakola, Ushetu (Ubagwe, Nonwe) na Shinyanga mjini, Dk. Slaa aliitaka Serikali ya CCM kuacha anasa za matumizi ya fedha ambazo zingeweza kuboresha miradi ya maendeleo, zikiwemo huduma za jamii kama maji, elimu na afya.

Alisema ni jambo la kushangaza na la kusikitisha kuona Rais akitumia fedha nyingi kiasi hicho katika safari za nje tu, wakati wananchi na watumishi wake kila siku wanalia na maisha magumu.

“Serikali inaingia katika anasa ya kutumia fedha katika safari za nje, wakati wananchi ni maskini, watumishi wa umma nao wanalia na maisha magumu, wamepigika, vikongwe nao wanauliwa kwa sababu wana macho mekundu ambayo yanatokana na kutumia kuni kwa ajili ya kupikia, hii inasikitisha sana.”

“Serikali inasema hakuna fedha za kutosha za kuboresha maisha ya Watanzania na ya kuongeza mishahara ya watumishi wake ambao wanalia kila siku mishahara yao midogo, lakini eti fedha za safari za nje zenyewe zipo, ni jambo la kushangaza sana,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa safari za nje kwa kiongozi wa nchi zina umuhimu wake, lakini ni lazima masuala kadhaa, ikiwemo tija inayopatikana katika safari hizo na kuona kipaumbele cha matumizi hasa kuboresha maisha ya Watanzania kwanza, badala ya kutumia fedha nyingi katika safari hizo.

CHADEMA kinaendelea kufanya ziara zake hizo za M4C- Operesheni Pamoja Daima, ambapo jana Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Slaa, walibadilishana maeneo ya ‘kushambulia’ ambapo Mbowe alitoka Geita kwenda Iringa, akiungana na Halima Mdee na Peter Msigwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Kati, huku Dk. Slaa akitoka Iringa kwenda Geita kuendelea na mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki na Magharibi.

Ziara za viongozi hao wa Chadema zimegawanyika katika makundi matatu, huku kaulimbiu ikiwa M4C- Pamoja Daima ambapo imebeba ajenda kadhaa ikiwa ni pamoja na mchakato wa Katiba Mpya, daftari la wapiga kura, rasilimali za nchi, kupanda kwa ugumu wa maisha, uchaguzi wa ndani wa chama hicho unaondelea katika ngazi ya msingi na uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 27 nchini.

No comments: