AS Monaco iliweka mezani kwake Pauni 10 milioni kuhakikisha anamshawishi Cristiano Ronaldo hadi anatua klabuni kwao. Lakini, Real Madrid ikamwambia atavuna pesa nyingi zaidi kama atamfanya staa huyo wa Ureno asaini mkataba mpya wa kubaki Santiago Bernabeu.
Akatazama masilahi, akamshawishi Ronaldo asaini na kubaki Bernabeu. Huyo ni Jorge Mendes, wakala makini wa wanasoka mwenye hadhi kubwa duniani.
Wakati hilo likitokea, Mendes, tayari alikuwa ameweka kibindoni pesa za maana kwa kuwezesha uhamisho wa wachezaji James Rodriguez, Joao Moutinho, Radamel Falcao na kocha Jose Mourinho.
Baada ya kufanikiwa kuliteka soka la Ureno kwa muda mrefu, Mendes amejijengea umaarufu mkubwa kwa wachezaji na makocha na hivyo kukubali kuwa chini yake.
Mendes, ambaye jina lake halisi Jorge Paulo Agostinho Mendesm alizaliwa Januari 7, 1966 huko Lisbon, Ureno anazungumza Kiingereza, Kifaransa, Kitaliano na Kihispaniola kwa ufasaha mkubwa. Anatembea na lundo la simu na shughuli yake inamfanya kulala saa chache sana.
Mendes mtaji wake ni wachezaji na anawamiliki zaidi ya wachezaji 100 wenye thamani zaidi ya Euro 500 milioni. Anavuna mamilioni ya pesa kila mwaka. Mendes ni tajiri mwenye pesa za maana.
Jinsi anavyopiga pesa
Mendes anamiliki kampuni yake ya uwakala wa wachezaji, GestiFute ambayo aliianzisha mwaka 1996. Wanasoka anaowamiliki ni Jose Mourinho, Luiz Felipe Scolari, Carlos Queiroz, Simao Sabrosa, Anderson, Fabio Coentrao, Pepe, Angel Di Maria, Cristiano Ronaldo, Radamel Falcao Garcia, Ricardo Carvalho, Nani, Ricardo Quaresma, Burak Yilmaz, Joao Moutinho, James Rodriguez, David de Gea na Victor Valdes Joao Pedro Oliveira.
Kwa kuwamiliki tu wanasoka hao unaweza kuona fursa za kipesa ambazo wakala huyo anakabiliana nazo. Mendes pia ndiye mtu aliyewafanya Wareno Ronaldo, Carvalho na Nani kupata mafanikio makubwa nje ya uwanja.
Dili lake la kwanza la uhamisho lilikuwa la Nuno wakati alipohama kutoka Vitoria de Guimaraes na kutua Deportivo de La Coruna. Alikutana na kipa huyo kwenye baa huko Guimaraes na uhamisho huo ulimpa heshima na kuwanasa wachezaji wa Kireno akiwamo Jorge Andrade.
Hugo Viana alipohama kutoka Sporting kwenda Newcastle United kwa Euro 12 milioni mwaka 2002, huo ulikuwa uhamisho wake wa kwanza mkubwa wa kimataifa na baada ya hapo akawahamisha Cristiano Ronaldo na Ricardo Quaresma.
Mwaka 2004, alimhamisha Mourinho kutoka FC Porto na kutua Chelsea, uhamisho huo ulimwingizia pesa nyingi. Dili hilo lilimpa pesa nyingi kwa sababu awali Mourinho aliripotiwa kutua Liverpool.
Chelsea walinogewa na Mendes na kumpatia pesa za maana baada ya kufanikisha pia uhamisho wa wachezaji Ricardo Carvalho, Paulo Ferreira, Tiago na Maniche klabuni hapo. Kwenye dili hizo, Mendes alivuna pesa pande mbili kutoka kwa wachezaji na klabu ya Chelsea.
Kampuni yake inamiliki haki za kiuchumi za wanasoka hao. Mwaka 2014, aliiuzia FC Porto asilimia 20 ya hisa ya umiliki wa mchezaji Deco na hilo limemfanya kuingiza Euro 2.25 milioni na asilimia tano ya hisa za Ricardo Carvalho na Paulo Ferreira.
Baadaye, GestiFute ilipiga bei hisa nyingine 15 za Deco na kuingiza Euro 1.25 milioni na hisa asilimia 10 za straika Benni McCarthy. Kwenye uhamisho wa Ferreira na Thiago, Mendes aliingiza Euro 2.9 milioni na Euro 2.25 milioni ikiwa pamoja na gharama za afya za wachezaji hao na gharama nyingine za mahitaji yao ya nje ya uwanja.
Mendes alivuna Pauni 4 milioni kwenye uhamisho wa Anderson alipotoka Porto kuhamia Man United sawa na kiwango alichovuna mwaka 2009 kwenye uhamisho wa Ronaldo kwenda Real Madrid kwa Pauni 80 Milioni.
Wakala huyo alifunga Euro 3.6 milioni pia kwenye uhamisho wa Bebe alipotua Man United.
Agombana na wakala wa Figo
Mendes alijikuta kwenye ugomvi mkubwa Uwanja wa Ndege wa Portela mjini Lisbon, Ureno dhidi ya wakala wa Luis Figo, Jose Veiga, baada ya kuona umaarufu wake unafunikwa.
Mwaka 2011 kampuni ya Mendes ya Gestifute ilijikuta kwenye ugomvi mkubwa na Kampuni ya Formation inayoongozwa na wakala wa Wayne Rooney, Paul Stretford. Formation ilipeleka kesi mahakamani ikiishtaki Gestifute kwa kucheza rafu kwenye uhamisho wa wachezaji nchini England.
Mendes aliingia kwenye ugomvi na mawakala wenzake kutokana na umahiri wake wa kudaka dili safi na wanasoka wake mara zote amekuwa akiwahamisha kwa pesa za maana na kuhakikisha wanavuna mishahara minono ili kuendelea kupata faida.
FC Porto ilipomuuza Falcao kwenda Atletico, GestiFute ilivuna Euro 3.7 Milioni, pesa ambazo zilimnufaisha Mendes moja kwa moja.
Mendes alikuwa mwanasoka, lakini hakuwa na bahati kwenye hilo baada ya kukataliwa na klabu mbalimbali za Ureno kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 20.
Baada ya kukwama kwenye soka kama mchezaji, Mendes alifungua sehemu ya kukodisha kanda za video kabla ya kufanya kazi kama DJ na baadaye alifungua baa na klabu ya usiku huko Caminha.
No comments:
Post a Comment