Thursday, 16 January 2014

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema kuwa jeshi la Uganda linashirikiana na wanajeshi wa Sudan kusini kupambana na waasi wa Sudan Kusini.

Mapigano hayo ambayo yalizuka mwezi uliopita yanaendelea katika maeneo kadhaa ya Sudan kusini, licha ya kufufuliwa kwa mazungumzo ya amani katika nchi jirani ya Ethiopia .
Taarifa zinazohusiana


Baada ya wiki kadhaa za tetesi za wanjeshi wa Uganda kuwa nchini Sudan Kusini, jeshi la Uganda sasa limekiri rasmi kuwa liko katika vita na waasi wa Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, Luteni Kanali Paddy Ankunda, Uganda ina takriban wanajeshi elfu moja na mia sita nchini humo.
Serikali ya Uganda imekiri kukabiliana na waasi hao tangu mwanzoni mwa wiki hii,wakati wanajeshi hao waliposhambuliwa na waasi wanaoongozwa na makamu wa zamani wa Rais Riek Machar.

Akisimulia kuhusu tukio hilo kwenye mkutano wa kikanda nchini Angola mnamo Jumatano, Rais Yoweri Museveni, alisema kwamba baadhi ya wanajeshi wake waliuawa au kujeruhiwa.

Jeshi la Uganda hata hivyo halijaeleza idadi kamili ya wanajeshi waliouawa.

Luteni Kanali Paddy Ankunda ametetea hatua ya Uganda kupeleka wanajeshi wake Sudan Kusini ikisema lengo lake ni kulinda raia na kufungua njia kwa misaada kuingizwa nchini humo .

Serikali ya Uganda imekuwa ikiunga mkono kikamilifu serikali ya Rais Salva Kiir ikisema kwamba imechaguliwa kidemokrasia wakati Riek Machar anataka kunyakua madaraka kwa nguvu.

Uganda ina maslahi nchini Sudan Kusini. Ni kituo rasmi cha kuuza bidhaa zake na kituo ambacho waasi wa Joseph Kony wamekuwa wakipigania na kutatiza serikali ya Museveni ingawa sasa wamedhibitwa

No comments: