Monday, 6 January 2014

Dunia yaomboleza kifo cha mchezaji nguli Eusebio

Mashabiki wa soka duniani wanaomboleza kifo cha mchezaji nguli alietawala soka la Ureno katika miaka 1960, Eusebio da Silva, "chui mweusi," alifariki dunia siku ya Jumapili akiwa na umri wa miaka 71

Marehemu Eusebio da Silva Ferreira.


Eusebio da Silva Ferreira, ambaye alifariki kutokana na ugonjwa wa moyo mapema Jumapili, alitawala soka la Ureno katikati mwa miaka ya 1960, na kuiletea heshima klabu yake ya Benfica na taifa lake. Kifo chake kimesababisha kumiminika kwa salamu za rambirambi, huku serikali ya Ureno ikitangaza siku tatu za maombolezi, ambapo bendera za taifa hilo mjini Lisbon zinapepea nusu mlingoti
Mashabiki wakiwema maua na vitambaa katika sanamu ya Eusebio iliyoko katika uwanja wa klabu ya Benfica mjini Lisbon, Ureno.

Amuagiwa sifa kemkem
Rais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani Sepp Blatter alisema katika mtandao wake wa twitter kuwa mchezo wa kandanda umepoteza mtu mashuhuri, lakini akaongeza kuwa nafasi ya Eusebio katika wachezaji mashuhuri haitapotea kamwe.

Naye mchezaji mashuhuri wa Uingereza Bobby Chalton, ambaye aliisaidia Manchester United kupata ushindi dhidi ya Benfica katika fainali ya kombe la Ulaya mwaka 1968, alisema ilikuwa heshima kwake kumfahamu Eusebio.

"Aliiwakilisha timu ya taifa kwa moyo usiyo na mipaka. Sote tunakumbuka siku alipoondoka uwanjani akiililia Ureno. Machozi ya Eusebio siku hiyo ni machozi yetu leo. Taifa linalia kwa kifo chake," alisema rais wa Ureno Anibal Cavaco Silva.

Kocha wa Chelsea ya Uingereza, Jose Mourinho, ambaye ni Mreno, amemtaja Eusebio kama mchezaji wa milele, wakati naye mchezaji nyota wa Real Madrid ya Uhispania na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, akisema Eusebio ni shujaa wa siku zote.

Eusebio alifunga jumla ya magoli 733 katika mechi 745, na alishindana na wachezji nguli wa wakati huo wakiwemo Pele, Alfredo Di Stefano na Charlton. Katika mahojiano mwaka 2011, akikumbuka machozi yake baada ya Ureno kushindwa na Uingereza katika nusu fainali ya kombe la dunia mwaka 1966, Eusebio alisema: "Nilikuwa mchezaji bora wa dunia, mfungaji bora duniani na barani Ulaya. Nilifanya kila kitu isipokuwa sikufanikiwa kushinda kombe la dunia."
Eusebio akifunga bao kwa kichwa wakati wa mechi ya nusu fainali ya kombe la dunia dhidi ya Uingereza mwaka 1966.

Kutoka umaskini hadi nyota wa dunia
Akianzia katika maisha ya chini kabisa katika koloni la zamani la Ureno Msumbiji, Eusebio aliibuka kuwa moja wa shambuliaji wanaohofiwa zaidi duniani, akichanganya kasi iliyofananishwa na ya chui na uwezo mkubwa wa kushambulia.

Akitokea familia ya maskini Eusebio aliezaliwa mwaka 1942 katika jiji la Maputo wakati huo likijulikana kam Lorenco Marques, alianza kupata umaarufu katika soka la Msumbiji akiwa na klabu ya Sporting Lourenco Marques, ambayo ina mahusiano na Sporting Lisbon ya Ureno.

Kutokana na ufundi wake wa kipekee, nguvu na rekodi yake ya kufunga mabao, haikuchukuwa muda mrefu kuanza kujulikana nchini Ureno, ambako alipewa majaribio Desemba 1960 na klabu ya Sporting Lisbon, lakini ilikuwa ni kilabu ya Benfica iliomsajili .

No comments: